CHEGE AAHIDI MAJI, KUFUFUA MICHEZO, AIRO, OCHELE,WATIA NIA WAMUOMBEA KURA UBUNGE JIMBO LA RORYA


Mgombea Ubunge jimbo la Rorya Jafari Chege akiwaomba kura wananchi wa Kata ya Roche wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea Udiwani.
Aliyekuwa mbunge wa Rorya Lameck Airo akimuombea Kura Jafari Chege katika uzinduzi wa kampeni za Mgombea Udiwani kata ya Roche
Mgombea ubunge kupitia CCM jimbo la Rorya Jafari Chege akifurahi wakati wa mkutano wa kampeni kata ya Roche
***
Na Dinna Maningo,Rorya 
Mgombea UbungeJimbo la Rorya kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jafari Chege amesema kuwa akichaguliwa kuwa mbunge kazi yake kubwa itakuwa ni kwenda kujenga hoja bungeni pamoja na kukumbusha utekelezaji wa yale yaliyopo kwenye Ilani ya CCM ikiwemo ya Zahanati kila Kijiji.

Akizungumza  leo kwenye uzinduzi wa kampeni za mgombea Udiwani kata ya Roche Ally Juma,mgombea huyo alisema kuwa  kazi kubwa ya mbunge ni kujenga hoja na kuzisimamia ili zifanyiwe utekelezaji  lakini piawenuatua kero mbalimbali zilizopo ndani ya jimbo.

"Rorya ina changamoto kubwa ya maji mimi nitajikita kuzungumzia sera na siyo kumzungumzia mtu,kwakuwa wananchi wanahitaji kuona mgombea wao anawaaeleza nini na kufahamu Sera zake,mimi ni kijana mwenye nguvu ambaye nitashughulikia kero kwa wakati.

"Wananchi wanahitaji kiongozi wa kuwaunganisha pamoja na siyo kiongozi anayewagawa,mkishatengana hakuna maendeleo, ukabila ulisemwa sana Rorya lakini nawashukuru wananchi mnajitahidi kuupinga ukabila na mimi naupinga na ndiyo maana nikawiwa kugombea ubunge ili tuungane katika kuleta maendeleo" alisema Chege.

Akizungumzia kero ya maji alisema kuwa vijiji vingi havina maji kikiwemo kijiji cha Migeko ambacho wananchi wanatembea km 20 kufata maji ziwa Victoria nakwamba atahakikisha kijiji hicho anakipa kipaumbele ili kisima kichimbwe wakati huo michakato mingine ya utatuzi wa maji ikiendelea.

"Nikiwa mbunge nitapitia miradi yote ya barabara kujua yenye changamoto  na kuhakikisha inaingizwa kwenye mipango na inakarabatiwa,nitahakikisha naondoa masharti magumu ya mipoko inayowakabili wanawake na vijana ikiwemo namna ya kuandika katiba na suala la uanzishaji wa akaunti",alisema Chege.

Mgombea huyo aliongeza kuwa kupitia Sera ya chama atamuomba Rais na chama chake kuwa na vyuo wiwili vya ufundi Rorya ili kurahisisha shughuli za wananchi lakini pia kukuza kipato cha wananchi wakiwemo vijana.

Kwa upande wa michezo alisema kuwa  lazima michezo irejeshwe Rorya kwakuwa ni sehemu ya kuzalisha vipaji na kuunganisha ushirikianao kwa wananchi na nakwamba inaleta hamasa kubwa kwa wananchi.

Mbunge wa jimbo la Rorya Lameck Airo anaemalizia muda wake wa ubunge ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni za mgombea Udiwani aliwaomba wananchi wakiwemo na wa vyama vya upinzani kumpigia kura Chege.

"Chagueni CCM,mimi sijawahi kuwabagua wapinzani nyie ni mashahidi kuna kata zilizokiwa na Madiwani wa Chadema nimechangia maendeleo ikiwemo kata ya Ikoma tumejenga shule 4 ,Kitembe nimeungana nao kupambana na wizi na michango mbalimbali mchagueni Rais Magufuli,mchagueni Chege na Diwani Juma, mnafahamu hata  Mwenyekiti wangu wa CCM Ochele akiwa Diwani hapa tumefanya mengi",alisema

"Hata nikiwa nje ya ubunge nitashirikiana nanyi,mkiniita kwenye shughuli zenu ziwe za mbunge au Diwani nitakuja msiwe na wasiwasi,nawashukuru wana Roche kwa miaka 10 sijawahi kupigiwa simu ya watu kuibiwa mifugo,naombeni tufanye uchaguzi kwa uungwana tusikilize sera za wagombea,sisi wana CCM hatuna nguvu za kupigana wala kuhamasisha kukatana mapanga kazi yetu ni kuwaombeni kura", alisema Airo.

Mgombea Udiwani kata ya Roche Ally  Juma aliwaomba wananchi kumpigia kura nakueleza kuwa kabla ya kuchukua fomu alifanya utafiti na kugundua changamoto mbalimbali ikiwemo ya adha wanayoipata wananchi juu ya ukosefu wa kituo cha kutolea huduma ya afya.

"Kilichonihamasisha ni kuhusu vituo vya avya,kuna zahanati ya Osiri na Ng'ope zilijengwa na wananchi lakini zimekuwa magofu watu wanaenda kutibiwa Kenya,nitakapokuwa kwenye vikao vya halmashauri nitalazimisha ili haya majengo yaweze kukamilika kwa wakati,lakini kwa mambo yatakayoshindikana  nitamweleza mbunge nae atayawasilisha bungeni", alisema Juma.

Mwananchi wa kijiji cha Roche Godwin Johson alimtaka mgombea ubunge na Udiwani kama wakishinda watatue kero ya maji na kujenga lambo la maji la kunyweshea mifugo,maji safi na salama kwa wananchi pamoja na zahanati ya afya huku waliotiania kugombea Udiwani wakiahidi kutoa ushirikiano.

Godfrey Obonyo ambaye ni mjumbe wa kamati ya siasa wilaya ya Ilala-Dar es Salaam alisema dhamira ya kuzunguka vijijini ni kuitafutia kura CCM.

Waliotia nia kugombea ubunge viti maalumu Irine Makongoro na Stella Odatt waliwaomba wananchi hususani  wanawake kuipigia CCM kwakuwa ndiyo chama kitakachowaletea maendeleo.

Walio tiania kugombea Ubunge jimbo hilo akiwemo Wambura Sasi na Leonard Otuoma walisema kuwa wataendelea kumuunga mkono Chege kuhakikisha anashinda.

Daud Wembe alisema "Tumekuja kuzungumza mambo ya misingi,aliyepewa kusimamia rasilimali za Taifa ni Rais wetu Magufuli na yeye ndiye kamsimamisha Chege awe mbunge wetu najua kampeni bado zinaendelea tutasema mengi",alisema Wembe.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi  (CCM)wilaya ya Rorya Charles Ochele aliwaomba wana Roche kuwapigia kura viongozi wa CCM bila kumsahau Chege na kwamba chama hicho kimejipanga kuhakikisha kinashinda.

Katika uzinduzi huo wanachama 6 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) walimkabidi Ochele kadi za chama hicho na kujiunga na CCM kwa madai kuwa Serikali inayoongozwa na John Magufuli imefanya mengi ambayo yamewavutia na hivyo kujiunga na CCM.
Kushoto ni mwenyekiti wa CCM wilaya ya Rorya Charles Ochele wakiwa kwenye mkutano Kata ya Roche
Kikundi cha akina mama wa kata ya Roche wakiimba wakati wa kampeni za CCM
David Wembe aliyetiania ya Ubunge Rorya akizungumza na wananchi wa kata ya Roche
Aliyekuwa Mtia nia Ubunge Leonard Otuoma  akizungumza na wananchi wa Roche

Irene Makongoro aliyekuwa mtiania ubunge viti maalumu akizungumza
Mwananchi wa Roche Godwin Jonson akizungumza
Aliyekuwa Mtia nia ubunge viti maalumu mkoa wa Mara Stella Odatt
Mgombea Udiwani kata ya Roche Ally Juma akiomba kura

Godfrey Obonyo mjumbe wa kamati ya siasa wilaya ya Ilala-Dar es Salaam akizungumza kwenye mkutano wa kampeni

Wanachama wa CHADEMA wakikabidhi kadi zao baada ya kuhamia CCM

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527