WAZIRI UMMY : NHIF TATUENI MALALAMIKO YA UPATIKANAJI WA BAADHI YA DAWA

Na.WAMJW,DSM

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) imetakiwa kutatua malalamiko ya upatikanaji wa baadhi ya dawa na vipimo kwa wananchi wenye bima ya afya.

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa kikao na Menejimenti ya Mfuko huo katika ofisi ndogo za wizara zilizopo jijini, Dar es Salaam.

“Kumekuwepo na malalamiko ya upatikanaji wa baadhi ya dawa na vipimo kwa watu wenye kadi za bima pia ucheleweshaji wa malipo ya watoa huduma za afya” Alisema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy ameutaka mfuko huo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na mfuko huo pamoja na mafao yanayotolewa katika vifurushi vya bima ya afya.

“Tatueni malalamiko yote kwa wakati ili wananchi wafurahie vifurushi vyote watakavyojiunga navyo”.Alisisitiza Waziri Ummy

Kikao hicho pia kiliangalia mwenendo wa utoaji wa huduma za bima za afya zinazotolewa na mfuko huo ambapo kilihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa NHIF, Benard Konga, Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, na Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527