WANACHAMA 323 WA CCM WAMERUDISHA FOMU KUGOMBEA UBUNGE MAJIMBO SITA YA SHINYANGA



Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Shinyanga Donald Magesa akionesha kitabu cha Kanuni na Maadili ya Uongozi CCM wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 18,2020 akitoa taarifa kuhusu wanachama wa CCM waliojitokeza kuchukua na kurudisha fomu kuomba kugombea nafasi ya Ubunge katika majimbo sita ya Mkoa wa Shinyanga ambayo ni Kishapu,Solwa, Msalala, Ushetu, Kahama Mjini na Shinyanga Mjini. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Shinyanga Donald Magesa akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 18,2020.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Jumla ya wanachama 324 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamejitokeza kuchukua fomu kuomba kugombea ubunge katika majimbo ya  Kishapu,Solwa, Msalala, Ushetu, Kahama Mjini na Shinyanga Mjini ambapo 323 ndiyo wamerudisha fomu.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari  leo Julai 18,2020 Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Shinyanga Donald Magesa amesema kati ya wanachama 324 waliochukua fomu mmoja pekee kutoka Jimbo la Ushetu hajarudisha fomu hivyo kufanya idadi ya waliorudisha fomu kuwa 323 kati yao wanawake ni 26, wanaume 297.

Magesa amefafanua kuwa kati ya wanachama wa CCM walioomba kugombea ubunge katika Jimbo la Kishapu ni 78 (wanawake wanne), Shinyanga Mjini 60 (wanawake 7), Solwa 54 (wanawake wanne), Kahama Mjini 70 (wanawake 8), Msalala 44 (wanawake wawili) na  Ushetu 18 (mwanamke mmoja).

Aidha amesema jumla ya wanachama 43 kupitia UWT walichukua fomu za kuomba kugombea nafasi ya Ubunge Viti maalum ambapo mmoja hajarudisha fomu, walioomba ubunge viti maalumu kupitia kundi la Vijana ni 14 na kupitia Umoja wa Wazazi waliochukua na kurudisha fomu ni watatu.

 Amesema mkutano wa kura za maoni kuwapigia kura wagombea utafanyika Julai 20,2020 huku akiwatahadhalisha wagombea kutojihusisha na vitendo vya rushwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527