VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA KUPEWA OFISI KWENYE JENGO JIPYA LA NEC- DODOMA


Viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa nchini watapatiwa ofisi katika jengo jipya la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) jijini Dodoma kwa ajili ya kufanya shughuli zao za kisiasa.

Pendekezo hilo limetolewa na Rais wa Tanzania, John Magufuli wakati akizundua jengo hilo la ghorofa nane linalojengwa na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA-JKT) eneo la Njedengwa jijini Dodoma.

“Nina uhakika katika jengo hili la ghorofa nane mtapanga maeneo vizuri angalau na sisi viongozi wa vyama mbalimbali tupate ofisi kwa sababu ni jengo la Watanzania,” amependekeza Rais Magufuli.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira, na Wenye ulemavu, Jenista Mhagama amesema kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania fomu za wagombea Urais zitatolewa jijini Dodoma na matokeo ya uchaguzi yatatangazwa kutoka huko.

Awali akizungumza kuhusu ujenzi wa jengo hilo Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage ameipongeza SUMA-JKT kwa kazi kubwa wanayofanya na amependekeza taasisi hiyo ipewe kandarasi nyingine za kujenga majengo ya serikali.

Katika hatua nyingine, Rias Magufuli ametoa muda wa wiki mbili kwa taasisi zote za serikali zinazodaiwa jumla ya shilingi bilioni 11 na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kulipa madeni yao vinginevyo atachukua hatua dhidi yao. Amesema haijalishi taasisi hiyo ni ipi, hata kama ni Ikulu au ofisi wa Spika wa Bunge, zinapaswa kulipa madeni.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post