MAKAMISHNA WA ARDHI WATAKIWA KUKUTANA NA TAASISI ZINAZODAIWA KODI YA PANGO LA ARDHI

Na Munir Shemweta, WANMM SUMBAWANGA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewaagiza Makamishna Wasaidizi wa ardhi katika ofisi za mikoa kukaa na taasisi za serikali zinazodaiwa kodi ya pango la ardhi kuangalia namna bora ya kulipa madeni wanayodaiwa.

Dkt Mabula alitoa agizo hilo jana mkoani Rukwa wakati akizundua rasmi ofisi ya ardhi ya mkoa ikiwa ni mfululilizo wa uzinduzi wa ofisi za ardhi katika mikoa mbalimbali nchini. Tayari ofisi saba za ardhi katika mikoa ya Tanga, Arusha, Manyara, Singida, Iringa, Njombe na Songwe zimezinduliwa.

Alisema, mkoa wa Rukwa una taasisi za serikali pamoja na watu binafsi ambao kwa ujumla wao wanadaiwa zaidi ya shilingi bilioni moja kiasi alichokieleza kuwa ni kikubwa na fedha yake ingeweza kutumika katika shughuli za maendekeo kama vile ujenzi wa hospitali au barabara.

Alizitaja baadhi ya taasisi za serikali zinazodaiwa kodi ya pango la ardhi katika mkoa wa Rukwa kuwa ni pamoja na Shirika la umeme Tanzania (Tanesco), Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Chuo Kikuu Huria na kubainisha kuwa katika kumuwezesha rais kufanya kazi ya shughuli za maendeleo kuna wajibu wa kulipa kodi ya pango la ardhi.

‘’Bilioni moja ni fedha nyingi sana nawaagiza Makamishna Wasaidizi wa mikoa kukutana na taasisi pamoja na watu wengine wanaodaiwa kodi ya pango la ardhi kukubaliana namna bora ya kulipa fedha wanazodaiwa vinginevyo taratibu za kisheria zitafuata’’ alisema Dkt Mabula

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Taasisi za serikali zinatenga fedha kwenye bajeti zake kwa ajili ya kulipia gharama mbalimbali ikiwemo kodi ya pango la ardhi na kutolipa kodi hiyo ni kutotimiza wajibu wa kulipa kodi ya ardhi.

Alisema, Wizara yake ilikutana na makampuni na taasisi za serikali zenye malimbikizo makubwa ya kodi ya pango la ardhi mkoani Dodoma na baada ya kukutana ndani ya mwezi mmoja zilikusanywa takriban bilioni ishirini na moja jambo linaloonesha kuwa taasisi hizo zinazo fedha kwa ajili ya kodi hiyo.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi Dkt Angeline Mabula alisema, wizara yake imeridhia kuanzishwa Baraza la Ardhi la Nyumba la wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.

Hatua hiyo inafuatia Dkt Mabula kuridhishwa na juhudi za wilaya ya Nkasi katika kuanzisha baraza hilo ambapo alikagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi yake katika eneo la Namanyele wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa na kusema kuwa kwa sasa takriban mabaraza mia moja ya ardhi ya nyumba ya wilaya yameidhinishwa lakini ni mabaraza 55 ndiyo yanayofanya kazi.

Hata hivyo, aliongeza kwa kusema kuwa, wakati mchakato wa ofisi za baraza hilo ukiendelea mwenyekiti wa baraza la ardhi la wilaya ya Sumbawanga anaweza kupanga ratiba na kwenda kuendesha mashauri ya migogoro ya ardhi kwenye wilaya ya Nkasi kwa lengo la kupunguza mashauri hao.

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa, mkoa wake una baraza moja tu la ardhi la nyumba na wilaya huku mkoa mzima ukiwa umesajili jumla ya mashauri 308 ya migogoro ya ardhi kuanzia mwezi januari hadi juni mwaka huu.

Alisema, kufuatia hali hiyo iko haja ya kuanzishwa baraza la ardhi la wilaya ya Nkasi kwa kuwa wananchi wa wilaya hiyo wamkuwa wakipata taabu kutembea umbali mrefu na wakati mwingine hulazimika kusafiri kilomita 160 kufuata huduma ya baraza wilayani Sumbawanga.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527