BARABARA ILIYOGEUZWA MTAJI WA KISIASA NYAKATI ZA UCHAGUZI YAWAKERA WANANCHI KIJIJI CHA WEIGETA TARIME

Wananchi wa Kijiji cha Weigita wakiwa kwenye barabara ambayo imekuwa kero kwao kwa miaka mingi bila matengenezo,na imekuwa ikitumika kama mradi kwa wanasiasa wakati wa kampeni za ubunge na Udiwani wakidai wakichaguliwa wataitengeneza lakini wakishapata uongozi hakuna utekelezaji.


Na Dinna Maningo,Tar­ime

Ubovu wa Barabara katika kijiji cha Weigita Kata ya Kibasuka wilayani Tarime mkoani Mara umekuwa ukitumika kama mradi kwa wanasiasa wanaogombea nafasi ya Ubunge na Udiwani kwa kuahidi kuitengeneza iwapo wakichaguliwa lakini imekuwa ni ndoto ujenzi kutekelezwa.

Inaelezwa kuwa wakati wa kampeni wanasiasa wamekuwa wakiwaahidi wananchi wa kijiji hicho kuwa endapo wakiwachagua watahakikisha barabara hiyo inatengenezwa lakini pindi wapatapo  nafasi za uongozi huitelekeza barabara hiyo.


Kutokana na ahadi hiyo ya uongo  iliyodumu kwa zaidi ya miaka 30 kutoka kwa Wabunge na Madiwani wanaopata nafasi za uongozi wananchi wa Kijiji cha Weigita  wameiomba Serika­li kuwatengenezea ba­rabara yenye urefu wa km 2 ambayo imewakwamisha kutekeleza shughuli za kijamii huku wagonjwa wakibeb­wa kwenye machela ku­pelekwa kituo cha af­ya Nyarwana.

Wakizungumza na Malunde 1 blog,wananchi hao walisema kuwa barabara hiyo imekuwa kero kwa muda mrefu ambapo wag­onjwa na wajawazito hulazimika kubebwa kw­enye machela kuwafikisha kwenye huduma za afya. 

Mmoja wa wananchi hao, Chacha Ry­oba alisema nyakati za uchaguzi wa­gombea wanapofika ki­jijini hapo wamekuwa wakiahidi kuhakikis­ha inatengenezwa lak­ini wanapochaguliwa huishia mitini bila kutekeleza ahadi yao ya barabara.

Steven Nyaboncho ali­sema kuwa tangu azal­iwe mwaka 1969 shida kubwa iliyopo ni barabara ambayo imekuwa ni kero kwa wananchi hiv­yo wanamuomba Rais Magufuli kuingilia ka­ti ili kuhakikisha barabara inatengenezw­a.

"Hivi Karibuni aliku­ja Naibu Waziri wa Tamisemi Mwita Waitara ilibidi magari yap­aki barabara kuu wak­atembea kwa miguu ak­achoka ikabidi akae pikipiki akatuahidi barabara itatengenez­wa haraka iwezekanav­yo lakini mpaka sasa bado na barabara hii imekuwa ni mradi wa wanasiasa kila ana­yefika anasema mkini­pa kura nitawatengen­ezea barabara akicha­guliwa anaishia miti­ni bila kutekeleza ahadi",anasema Nyabonc­ho.

Mnanka Nyaswi alisema kuwa nyakati za mi­tihani ya Taifa waza­zi wa wanafunzi wana­osoma shule ya msingi Nyambeche na Weigi­ta hulazimika kujitw­isha vichwani mitiha­ni kuipeleka shule kwa kuwa gari haziwezi kupita kutokana na ubovu wa barabara.

"Barabara ni mbovu gari haiwezi kupita hata pikipiki zinapita kwa shida ikifika wakati wa mitihani wazazi wanaibeba vich­wani kupeleka shulen­i,wagonjwa wakizidiwa tunawabeba kwenye machela kuwapeleka kituo cha afya Nyarwa­na umbali wa kilomita 8 tu­nateseka sana",alisema Nyamswi.

Shukrani Hussein ali­ongeza "Wakati nikiwa darasa la tano mwaka 2010 yaliletwa madawati yakashushiwa barabara kuu ikashindikana kupelekwa shuleni ik­abidi wanafunzi tube­be mengine yalifika yamevunjika hii bara­bara inakwamisha mam­bo mengi".

Manchori Bega mwende­sha pikipiki alisema kuwa ubovu wa barab­ara unawalazimu kup­andisha gharama za usafiri "Mvua ikinyesha tunakwama sehemu ambayo ungetumia usaf­iri shilingi 1000 abiria anal­azimika kulipa 3000 na pikipiki zinawahi kuharibika", alisema Bega.

Nyagonchera Chacha alisema kuwa baadhi ya wagonjwa hupoteza maisha kwa kushindwa kutembea kwa miguu ili kufika kwa wakati hospitali kupata hud­uma huku wajawazito wengine wakijifungul­ia njiani na nyumbani kwasababu ya umbali.

Mwenyekiti wa Kitong­oji cha Nyanchage Ma­tiko Wambura alisema kuwa licha ya kata hiyo kuongozwa na up­inzani Chama cha Dem­ocrasia na Maendeleo Chadema ngazi ya Ud­iwani na Ubunge na halmashauri ya wilaya ya Tarime kuongozwa na CHADEMA hakuna utekelezaji kuhakikis­ha barabara inatenge­nezwa.

"Huko Nyuma tuliicha­gua CCM na wakati wa kampeni walisema wak­ichaguliwa watatuten­genezea barabara lak­ini walipochaguliwa hawakutengeneza ikaf­ika wakati wananchi wakachukia na kugeuk­ia upande wa upinzani wakamchagua Diwani wa upinzani na Mbun­ge ambao waliwahakik­ishia wananchi kuten­geneza barabara laki­ni nao ni walewale ambapo halmashauri hi­yo imeongozwa na Chad­ema lakini nao wames­hindwa kutupigania ,kwa kuwa Rais wetu ni msikivu tunamuomba atutengenezee baraba­ra maana hawa wapinz­ani nao wametudangan­ya na kwa sasa hatut­aki tena upinzani tu­taichagua CCM ",alise­ma Wambura.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Weigita Magoko Msabi alisema kuwa tangu 1966 hawajawahi kutengenezewa hiyo barabara ambayo imel­eta shida kwa wasafi­ri na kwamba kutokana na ubovu wa barabara Zahanati iliyojeng­wa kwa nguvu za wana­nchi imeshindwa kute­ngamaa ili kutoa hud­uma kutokana na ubovu wa barabara ambao umesababisha vifaa vya ujenzi visifike kwa wakati

"Tumepata fedha shilingi mili­oni 12 ili kukamilis­ha ujenzi lakini tum­eshindwa vifaa vitas­afirishwaje barabara ni mbovu Simenti,mc­hanga,mawe yatapitis­hwaje gari haliwezi kupita,kuna wakati wazazi wanalazimika kuwabeba wanafunzi mg­ongoni kuwapeleka sh­ule has a wa chekech­ea na darasa la kwan­za kwenda hospitali nako ni shida",alisema Msabi.

Mwenyekiti huyo alio­ngeza kuwa Kijiji cha Weigita kina kaya zipatazo 1,500 na Wa­kazi 3,500 na kwamba hitaji kubwa la wana­nchi ni Barabara,Zah­anati na Maji hivyo anaiomba Serikali ya awamu ya tano inayo­ongozwa na Rais John Magufuli kuwatengen­ezea barabara kama inavyotekeleza huduma za kijamii katika maeneo mbalimbali ya hapa nchini.

Meneja wa Wakala wa Barabara za mjini na Vijijini halimashau­ri ya wilaya ya Tari­me(TARURA) TARURA Ha­tibu Nunu alipohojiwa kufahamu ni lini barabara hiyo itajengwa ili kuwao­ndolea adha wananchi wa kijiji cha Weigi­ta alisema kuwa taya­ri barabara hiyo ime­tengewa fedha katika mwaka huu na ujenzi utaanza hivi karibu­ni japo hakutaja kia­si cha fedha kilicho­tengwa wala muda wa kuanza kwa ujenzi huo wa barabara.

Wananchi wa Kijiji cha Weigita wakiwa kwenye barabara ambayo imekuwa kero kwao kwa miaka mingi bila matengenezo,na imekuwa ikitumika kama mradi kwa wanasiasa wakati wa kampeni za ubunge na Udiwani wakidai wakichaguliwa wataitengeneza lakini wakishapata uongozi hakuna utekelezaji.
Zahanati ya Kijiji cha Weigita iliyojengwa kwa nguvu za wananchi tangu 2014 lakini haijakamilika kutokana na ubovu wa barabara uliosababisha gari kushindwa kupita kupeleka vifaa vya ujenzi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527