DKT.SHEIN : SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR (SMZ) INATEKELEZA HAKI ZA BINADAMU KWA KUTOA AFYA NA ELIMU BURE

Na.Mwandishi Wetu-MAELEZO

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali inatekekeleza utawala bora kwa wananchi kwa kuwapatia huduma za jamii zikiwemo elimu na  afya zinazotolewa bure.

 Akizungumza alipokutana na ujumbe wa watendaji wa juu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Ikulu Zanzibar, Dkt. Shein alisema kuwa Serikali inatakeleza kwa vitendo dhana ya utawala bora ikiwa ni utekelezaji wa dhana iliyoasisiwa na Hayati. Abeid Aman Karume baada ya Mapinduzi ya Mwaka 1964.

“Lengo kuu la mapinduzi wakati huo lilikuwa ni kuhakikisha haki za binadamu zinatekelezwa kwa kila mwananchi hapa Zanzibar, kwa hiyo Hayati. Abeid Aman Karume aliiongoza Zanzibar kulete haki hizo ikiwemo elimu, afya na ardhi ambapo kabla ya hapo huduma zilikuwa zinatolewa kwa madaraja, hasa sekta ya afya na elimu daraja A lilikuwa la Waingereza, B lilikuwa la zile familia za kisultani, C watu wa katikati na D watu wa kawaida ambao kimsingi walikuwa wanapata huduma mbovu, kwa hiyo suala la utekelezaji wa haki za binadamu lina historia kwa hapa Zanzibar”, alisema Dkt.Shein.

Alibainisha kuwa baada ya Mapinduzi wananchi walianza kupata haki zao za msingi ikiwemo elimu, kuanzia darasa la kwanza hadi la nne na kuanzia darasa la tano kulikuwa na malipo ambayo yalimnyima mwananchi wa hali za chini haki hiyo.

 Kwa upande wa ardhi, Dkt. Shein alisema kuwa ilikuwa ni ngumu kwa wananchi wa Zanzibar kumiliki ardhi kabla ya mapinduzi kwani ardhi iligawiwa kwa wageni na wenyeji kuwa wafanyakazi wa mashamba ya wageni, lakini baada ya mapinduzi kila mwananchi alikuwa na uhuru na haki ya kutumia ardhi kwa mujibu wa sheria.

Alifafanua kuwa mambo hayo matatu ni ishara ya kwamba SMZ imeanza utekelezaji wa Utawala bora na Haki za Binadamu mara tu baada ya kuidai haki  hiyo kwa wakoloni, na hii ilileta furaha kwa kila Mzanzibar kupata haki zake za msingi kama vile ardhi, afya na elimu bure amabapo mpaka sasa Serikali inatoa huduma hizo bure kwa asilimia 100.

Naye, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu amesema kuwa chini ya Uongozi wa Rais. Shein utawala bora na utekelezaji wa haki za binadamu umeonekana wazi  kwa kuwa hadi  sasa Serikali yake inatoa huduma za afya na elimu bure kwa kila mwananchi.

“Mhe. Rais kutokana utekelezaji wa utawala bora na  haki za binadamu,  Zanzibar imeendelea kuwa na amani, lakini pia wananchi wameendelea kupata huduma za afya na elimu bure, hii ndiyo dhana ya utawala bora”, Jaji Mwaimu.

Alibainisha lengo la kumtembelea kuwa  ni kuweka ukaribu na Serikali yake ikiwa ni pamoja na kutekeleza majukumu ya tume hiyo ambayo   ni kufuatilia utekelezaji wa haki za  msingi za wananchi.

Aidha, Jaji Mwaimu aliipongeza SMZ kwa kushughulikia vizuri janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona, kwani  Serikali hiyo ilikuwa bega kwa bega na  wananchi kwa kuwapa moyo wa kufanya kazi huku wajikinga na maradhi hayo na mpaka sasa janga hilo limepungua kwa kiasi  kikubwa.

“Serikali imechukua  hatua kubwa kushughulikia janga la corona na tunashukuru kwamba viongozi wote wa pande zote mbili mmekuwa na busara kubwa kwenye mapambano hayo pamoja na maagizo yaliyokuwa yanatolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ikiwemo kufungia watu ndani, lakini nyinyi mlisema watu wafanye kazi na sasa tumeshinda”, Jaji Mwaimu.

Mwisho


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527