REDESO, OXFAM ZASHIRIKI MAPAMBANO DHIDI YA CORONA KISHAPU


Na Sumai Salum - Kishapu
Mashirika yasiyo ya Kiserikali OXFAM na REDESO  yanayotekeleza mradi wa kupunguza athari za maafa (KAMA) wilayani Kishapu yamekabidhi vifaa   vyenye thamani ya shilingi Milion 37.2 kwa ajili ya kujikinga na maambukizi dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu  unaosababishwa na virusi vya Corona katika wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na magauni maalumu ya kuhudumia wagonjwa 208, viatu 58,kofia 58, barakoa 1,200 aina ya N95, barakoa aina ya surgical masks 970 pamoja na vidonge vya vitakasaji makopo 11.
Akipokea vifaa Juni 16,2020 hivyo mkuu wa wilaya ya Kishapu Mhe. Nyabaganga Talaba amewashukuru wadau hao kwa jitihada ambazo wamekuwa wakiendelea kuzifanya ndani ya wilaya.
 “Tunawashukuru wadau wetu tulionao kwenye wilaya yetu kwani wamekuwa mstari wa mbele kwa kushirikiana na serikali kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona ,tunawashukuru kwa msaada wa vifaa hivi ambapo   wahudumu wetu wa afya kuwa na uhakika na utoaji huduma kwani nao wamepata kinga hivyo.
 Ningependa kuendelea kuwaambia OXFAM na REDESO wasichoke kujitoa na kushirikiana nasi pale ambapo tutakapowahitaji”,alisema Talaba.
Akizungumza niaba ya shirika la OXFAM la mratibu miradi kanda ya ziwa Valentine Shipula alisema kuwa wanaowajibu wa kusaidia hospitali za wilaya kwa ajili ya kujiandaa na kukabiliana na ugonjwa huo kwa kutoa vifaa kinga ili pindi maafa yatakapotokea wahakikishe wanayakabili ikiwa ndiyo lengo la miradi yao nchini Tanzania ikiwemo wilaya ya Kishapu.
“Tumeona ni vizuri na sisi kama OXFAM kusaidiana kwa kushirikiana na nguvu ya serikali katika kupambana dhidi ya janga hili la Corona kwani ni mojawapo ya majanga ambayo yanaangaliwa kwa ajili ya kupunguza athari za maafa na hasa ikiwa ni miongoni mwa majanga yanayoleta maafa”alisema Shikula.
Kwa upande wake Meneja na Msimamizi wa Miradi wa Shirika la REDESO wilaya ya Kishapu Charles Bulegeya alisema kuwa wako tayari kushirikiana na serikali katika kuhakikisha Kishapu iko salama katika kila nyanja za maisha na ameshukuru kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakiupata kutoka kwa watumishi wa serikali pamoja na wananchi katika maeneo yao ya mradi.
Mradi wa kupunguza athari za  maafa (KAMA) nchini Tanzania ulianzishwa tangu mwaka 2017 unafanya kazi ndani ya wilaya tatu (3) mkoani Shinyanga ni wilaya za  Kishapu na Kahama na mkoani Kigoma uko wilayani Kibondo ukifadhiliwa na serikali ya nchini Ubergiji kupitia shirika la OXFAM Ubelgiji wenye lengo la kupunguza athari za maafa.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post