RAIS MAGUFULI AAGIZA WANAOGAWA BARAKOA ZISIZOTHIBITISHWA WASHUGHULIKIWE


Rais wa Tanzania, Dkt.  John Magufuli amewaagiza viongozi katika maeneo mbalimbali nchini kuwakamata na kuwahoji wale wote wanaogawa barakoa kwa wananchi ili waeleze zimethibitishwa wapi kuwa zinafaa kutumika.

“Ukimuona mtu anagawa barakoa kwa wananchi, ashikwe akaulizwe zimethibitishwa wapi,” amesema Rais Magufuli wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT).

Aidha, amewataka wananchi kuwa makini kwa kutokupokea barakoa ambazo hawajui mgawaji amezitoa wapi kwani vifaa hivyo vinaweza kutumiwa kusambaza virusi vya corona.

“Tusidanganywe kwa kuletewa mabarakoa ambayo hatujui yametoka wapi, tutaeneza corona bila sisi kujua. Anapokuletea mtu barakoa hujui hata ameitoa wapi kataa, mwambie kavae wewe na mke wako na watoto wako nyumbani.”

Amewasihi wananchi wanaotaka kuvaa barakoa washone wenyewe kwani watakuwa na uhakika wa usalama wake.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527