MSAJILI: VYAMA VYOTE VINA HAKI SAWA KUSHIKA DOLA


Na Mwandishi Wetu,MAELEZO

OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini imesema ruzuku sio kigezo cha Chama Cha Siasa kuwa na nguvu ya kushika dola na vijenge  hoja na ushawishi  itikadi yake kwa wananchi katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani Oktoba mwaka huu.

Rai hiyo imetolewa leo (Jumanne Juni 30, 2020) Jijini Dar es Salaam na Naibu Msajili wa Vyama Vya Siasa Nchini, Mohamed Ahmed wakati wa kufunga kikao kazi cha kuwajenga uwezo Viongozi wa Vyama vya Siasa na kusema  vyama vyote vipo sawa kwa mujibu wa sheria.

Ahmed alisema katika kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu, Vyama vya Siasa nchini havina budi kujitazama na kujikosoa kwa hoja zilizo imara zenye uwezo wa kuwashawishi wanachama wake katika msingi wa kushika dola baada ya kutazama ruzuku, kwani wakati wa kuanzisha mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992, vyama hivyo havikuwa na uwezo wa kifedha.

‘Ukitazama Vyama vya siasa vya mwaka 1992 sio vya leo, tulianza tukiwa wachanga kabisa na kushiriki katika chaguzi mbalimbali na leo hii vimeanza kujijenga siku hadi siku, tuvijenge vyama vyetu kwa ajili ya ushindani wa hoja katika uchaguzi na kushika hatamu ya uongozi’’ alisema Ahmed.

Aliongeza vyama voyte vyenye usajili wa kudumu vina haki sawa kwa mujibu wa sheria na kuwa hata vyama vyenye uwezo wa ruzuku vimejikuta vikiingia katika migogoro ya mara kwa mara baina yao na kuathiri dhana ya msingi mkuu wa vyama vya siasa, ambayo ni kushika hatamu ya uongozi na kuongoza dola.

Akifafanua zaidi alisema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itaendelea kushikiana na vyama vyote vya siasa katika kuwajengea uwezo katika kipindi hiki cha kuelekea katika Uchaguzi Mkuu kwa kupokea maoni, changamoto na kuendesha mikutano ya mara kwa mara na wadau wa siasa.

Aidha Ahmed alivikumbusha vyama vya siasa kuendeleza dhana ya uvumilivu, mshikamano na ushirikiano baina yao na kushindana kwa hoja na kuepuka tofauti za itikadi za siasa, upinzani, kwa kuwa nchi ndiyo kipaumbele cha kwanza katika jamii yenye amani na utulivu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Chama Cha Mapinduzi (CCM) Anna Abdallah aliipongeza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kuitisha mkutano huo kwa kuwa umetoa fursa kwa vyama hivyo kufahamu wajibu wa msingi wa vyama vya siasa katika kushiriki katika maendeleo ya nchi.

Anna alisema mkutano huo umetoa taswira halisi ya mtazamo wa vyama vya siasa na nafasi ya wananchi katika kufanya uamuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu wajibu na haki yao ushiriki wao katika maendeleo ya nchi na kuvikumbusha vyama hivyo kuwa siasa sio uhasama.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Nchini, John Shibuda alisema suala la amani na utulivu ni jambo muhimu linalopaswa kupewa kipaumbele na mamlaka na taasisi mbalimbali za dola katika kipindi hiki cha kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

‘Mwezi Julai tunatarajia kuwa na kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa, ambapo tutakutana na mamlaka za dola ikiwemo Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ili kuweza kuwekana sawa na kujitafakari sote kwa pamoja nafasi tuliyonayo kuelekea katika Uchaguzi Mkuu’’ alisema Shibuda.

MWISHODownload/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527