KATIBU MKUU WIZARA YA KILIMO AVITAKA VYUO VYA MAFUNZO YA KILIMO VIHUISHE MITAALA ILI IENDANE NA MAHITAJI YA NCHI


Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bwana Gerald Kusaya amewaasa Wakuu wa Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo vya Serikali na Binafsi Wana wajibu wa kuhuisha mitaala ya mafunzo ili iendane na mahitaji ya nchi ya sasa ambayo ni kuandaa wataalam ili wazalishe kwa tija kulingana na uchumi wa viwanda.

Katibu Mkuu Kusaya ameyasema hayo leo (30.06.2020) wakati wa mkutano aliouitisha Mjini Morogoro kwa ajili ya kukutana wa Wakuu wa Vyuo vya Mafunzo vya Serikali (Vyuo 14) na Wakuu wa Vyuo Binafsi (Vyuo 15) nchi nzima; lengo ni kuboresha utoaji wa mafunzo ya kilimo katika Tanzania ya viwanda.

Bwana Kusaya katika hotuba yake amewaeleza Wakuu hao wa Vyuo vya kuwa Wizara ya Kilimo ina lengo la kuongeza tija na uzalishaji katika Sekta ya Kilimo na kuongeza kuwa mchango wa Sekta ya Kilimo kwenye pato la taifa ni asilimia 28 ambapo mchango wa sekta ndogo ya mazao ni asilimia 16. 

Mchango huo unaweza ukaongezeka ikiwa Vyuo vya Mafunzo vya Serikali na Binafsi vitazalisha Wagani bora na siyo Wagani mizigo alisema Kusaya.

“Lengo hapa ni kuhakikisha mafunzo yatolewayo katika Vyuo hivi yanakuwa ni yale yanayo kwenda sambamba na hali ya sasa ya mahitaji ya maarifa katika Sekta ya Kilimo kwa kuondokana na mtindo wa kutumia mitaala iliyopitwa na wakati”. Amekaririwa Katibu Mkuu.

Bwana Kusaya ameongeza kuwa, tija na uzalishaji kwenye Sekta ya Kilimo inachangiwa na aina ya Wagani wanaozalishwa na Vyuo vya Mafunzo.

“Tunapokuwa na Wagani wenye weledi, ni dhahiri kuwa Sekta ya Kilimo inaweza kukua na kutoa mchango mkubwa kwa pato la Taifa. Kwa sasa Sekta ya Kilimo inachangia asilimia 28 ya pato la Taifa ambapo sekta ndogo ya mazao inachangia 16.2% ya pato la Taifa”.

“Ni muhimu sana kwa Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo; kujikita katika kuinua Sekta ya Kilimo kupitia mafunzo kwa vitendo na kubuni teknolojia ambazo zinaweza kumsaidia Mkulima. Vyuo vinapaswa pia kuwa chachu ya kueneza ubunifu kwa Wanafunzi ili waweze kuwa na maarifa na ujuzi wa kujiajiri.” Amekaririwa Bwana Kusaya.

Katibu Mkuu Bwana Gerald Kusaya ameongeza ili Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo vya Serikali na Binafsi viende sambamba na kasi ya mabadiliko ya hali ya ukuaji wa uchumi wa nchi ni vyema kuwe na ushirikiano na Wdau mbali ndani na nje ya nchi.

“Katika kufanya hayo yote Wakuu wa Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo wanapaswa kushirikiana na Wadau wengine wa maendeleo katika kuboresha teknolojia na mbinu za ufundishaji.”

“Kupitia Wadau mabalimbali; tumesikia wenyewe kupitia maelezo ya utangulizi namna ambavyo wameboresha mazingira ya ufundishaji Vyuoni, pia kushiriki katika uhuishaji wa mitaala na kuwajengea uwezo Wakufunzi katika nyanja za mbinu za ufundishaji.” Amesisitiza Katibu Mkuu.

Kipekee Katibu Mkuu Bwana Gerald Kusaya amewashukuru Wadau wa maendeleo ambao ni Viongozi na Wafanyakazi wa Mashirika ya Sustainable Agriculture Tanzania (SAT) na Lutheran World Relief (LWR). 

“Nimeelezwa kwamba, Mashirika haya yamekuwa mstari wa mbele kwa kufanya kazi za kuimarisha taaluma na mafunzo katika Vyuo vya Mafunzo ya kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo (Serikali) ili kufikia adhma ya kuwa na mitaala bora ya kufundishia kwa sasa na endelevu”. Amemalizia Katibu Mkuu.

Mwisho Katibu Mkuu aliwakaribisha Wadau wote; kwenda ofisini kwake kwa ajili ya mazungumzo yenye lengo la kuboresha na kuleta ufanisi katika maendeleo ya ugani na mafunzo ya kilimo.

Naye Dkt. Wilhelm Mafuru, Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo, Huduma za Ugani na Utafiti, Wizara ya Kilimo amesema maboresho ya mitaala katika Vyuo Mafunzo vya Serikali na Binafsi imehuishwa na itaendela kuhuishwa ili kuwaanda Wanafunzi na Wahitimu kujiajiri na si kufikiria kuajiriwa.

“Napenda kuwahakikishia Watanzania kuwa mbinu za kisasa za ufundishaji na uhuishaji wa mitaala ni jambo endelevu; Sambamba na maelekezo ya Katibu Mkuu; Tutaendelea kushirikiana na Wadau wote na mfano mzuri ni mkutano kama huu aliouitisha Katibu Mkuu.”Amekaririwa Dkt. Wilhelm Mafuru, Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo, Huduma za Ugani na Utafiti, Wizara ya Kilimo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post