DALADALA DAR RUKSA KUSIMAMISHA WANAFUNZI WANNE

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameagiza daladala za mkoa huo, ziruhusu wanafunzi wanne kusimama ili kuondoa changamoto ya usafiri.


Makonda alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam wakati akipokea vifaa tiba na vifaa vya ujenzi na kueleza kuwa, agizo hilo la kubeba wanafunzi lianze mara moja.

“Sitaki kusikia mwanafunzi anaachwa eti konda na dereva wanasema wanabeba abiria kulingana na viti, wabebwe ili waende kwenye masomo,” alisema.

Alisema daladala litakalokuwa limebeba wanafunzi wasiozidi wanne, trafiki haruhusiwi kulikamata, lakini kama amesimamisha abiria wachukue hatua.

Pia, alisema alitoa maelekezo ya bodaboda na bajaji kuingia katikati ya jiji kubeba abiria, lakini kuna mtu mmoja ameanza kuwakamata na kumweleza kuwa hakuna Mkuu wa Mkoa mwingine.

“Hakuna Mkuu wa Mkoa mwingine, nipo na bado nipo, bodaboda, bajaji mnaendelea kuingia katikati ya mji kuendelea na shughuli zenu za kiuchumi kama nilivyoelekeza kauli hii sijaitengua na hakuna mwingine wa kuitengua katika mkoa huu labda mamlaka nyingine kutoka juu yangu,” alisema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527