WATU 7 WANAODHANIWA KUWA MAJAMBAZI WAUAWA DAR ES SALAAM

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kuwaua majambazi saba na kufanikiwa kukamata silaha ndogo Bastola aina ya BERETA ikiwa na risasi tatu ndani ya kasha (magazine) na silaha za jadi.Mnamo tarehe 25.05.2020 majira ya saa sita na dakika kumi usiku huko maeneo ya Mwenge Coca Cola majambazi saba wakiwa kwenye gari namba T 956 BYA Toyota Noah Rangi ya fedha (Silver) wakielekea kufanya uhalifu katika ghala la GS Group Limited linalohifadhi vifaa vya pikipiki, kabla hawajafanikiwa kufanya uhalifu huo.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum DSM kupitia kikosi kazi chake cha kupambana na ujambazi lilipata taarifa kutoka kwa msiri na kufika mara moja eneo la Mwenge Cocacola na kulibaini gari hilo, ambapo kikosi kazi hicho kilipojaribu kulifuata gari hilo la majambazi liliongeza mwendo na kuchepuka barabara ya vumbi na ghafla majambazi hao walianza kulishambulia gari la Polisi kwa risasi na ndipo askari wakajibu mapigo na kufanikiwa kupiga tairi gari la majambazi hao, majambazi hao wakashuka na kuanza kukimbia huku wakirusha risasi ovyo lakini askari Polisi kwa umahiri wa hali ya juu walifanikiwa kuwajeruhi majambazi wote saba na kufanikiwa kuwakamata wote.

Aidha katika upekuzi wa awali ndani ya gari la majambazi hao kuilikutwa na mitungi miwili ya gesi na mipira yake, Mapanga matatu, Kamba za katani (kudu) na baada ya kumpekua jambazi mmoja alikutwa na silaha ndogo Bastola aina ya BERETA ikiwa na risasi tatu ndani ya kasha (Magazine).Majambazi wote saba walikimbizwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na walipofikishwa hospitalini hapo daktari alithibitisha kuwa wameshafariki dunia na miili yao imehifadhiwa hospitalini hapo kwa uchunguzi zaidi.

TATHIMINI YA HALI YA USALAMA KATIKA KUISHEREKEA SIKUKUU YA EID EL-FITRI JIJI DAR ES SALAAM.

Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama limefanikiwa kuimarisha usalama kipindi chote cha kusherekea sikukuu ya Eid-El-Fitri Jijini DSM na kwamba hakuna tukio lolote la uhalifu lililoripotiwa au ajali mbaya ya barabarani iliyoripotiwa.

Sikukuu hiyo ya Eid-El-Fitri iliyosherekewa Tarehe 24.05.2020 na kuendelea tarehe 25.05.2020.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum DSM limejipanga kikamilifu kuhakikisha inasherekewa kwa amani na utulivu maeneo yote ya Jiji la Dar es Salaam na linawataka wananchi kuendelee kufuata sheria za Nchi ili kumalizia kusherekea sikukuu hii kwa amani na utulivu.

Imetolewa na
Kamanda wa Polisi,
Kanda Maalum ya Dar es Salaam,

SACP-Lazaro Mambosasa,
25/05/2020


Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527