SERIKALI YASEMA DEMOKRASIA ITAENDELEA KUHESHIMIWA NCHINI

Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Dodoma

Serikali inaendelea na zoezi la Kidemokrasia la wananchi kuboresha taarifa za wananchi kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga Kura ambazo zitatumika kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Mdiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2020.

Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi ameongoza zoezi hilo kwa Makatibu Wakuu leo Mei 04, 2020 hapa jijini Dodoma kuhakiki na kuhuisha taarifa zao katika ikizingatiwa leo ni siku ya mwisho kwa zoezi hilo nchini kote.

“Serikali inaendelea kukamilisha kuboresha Daftari la Kudumu la Mpiga Kura, Serikali zoezi hili ni muhimu sana kwa nchi yetu ikizingatiwa ni la kidemokrasia licha ya kwamba nchi yetu na dunia nzima inapitia kwenye changamoto tuliyonayo ya COVID-19” alisema Dkt. Abbasi.

Ameongeza kuwa Demokrasia itaendelea kuheshimiwa nchini kwa sababu ni kitu muhimu sana na viongozi hao pamoja na wananchi waliojiandikisha kutumia haki yao ya Kikatiba kuchagua viongozi wao.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome amesema kuwa Wizara yake inajukumu la kuhamasisha mambo mbalimbali ikiwemo elimu ya haki ya Mpiga kura.

“Nchi yetu imepiga hatua kubwa sana katika demokrasia kiasi kwamba tunajivunia hatua tuliyofika ni nzuri na demokrasia imekuwa ni ya kweli hakuna mwaka ambao tumevuka miaka mitano hatujafanya uchaguzi na wanannchi wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kuwachagua viongozi wao” alisema Prof. Mchome.

Lengo la elimu ya mpiga kura ni kuwahamasisha wananchi kutumia haki yao ya kikatiba katika kujitokeza na kushiriki kuchagua viongozi wao watakao waongoza ili kujenga Demokrasia na Utawala Bora nchini hatua inaanza kwa wananachi kijiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga Kura ambalo linaratibiwa na kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post