MAMA AMUUA MTOTO WAKE KISHA KUMZIKA MWENYEWE MVUA IKINYESHA KISHAPU

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Mwanamke aliyejulikana kwa jina la Lucia Lukenya Mahizi (42) mkazi wa Kitongoji cha Wizunza kijiji cha Seke Ididi kata ya Sekebugoro wilayani Kishapu mkoani Shinyanga anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumuua kisha kumzika mtoto wake mwenye umri wa siku mbili kwa madai kuwa ni ugumu wa maisha baada ya kutelekezwa na aliyempa mimba.Akitoa taarifa kwa Vyombo vya Habari leo Alhamis Mei 28,2020 Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema mtuhumiwa amekamatwa Mei 26,2020 baada ya wananchi kubaini kuwa mwanamke huyo hana mtoto aliyejifungua. 

“Tunamshikilia Lucia Lukenya Mahizi (42) mkazi wa kitongoji cha Wizunza kijiji cha Seke Ididi kwa kosa la mauaji ya mtoto wake mchanga, jinsia ya kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa siku 02 baada ya kuzaliwa kwake kisha kumzika mwenyewe pekee yake wakati mvua kubwa ikiendelea kunyesha ili watu wasimuone”,amesema Kamanda Magiligimba. 

Akisimulia kuhusu tukio hilo Kamanda Magiligimba amesema tarehe 26.05.2020 majira ya saa kumi na mbili jioni (12:00) katika maeneo ya kitongoji cha Wizunza kijiji cha Seke Ididi wananchi wa maeneo hayo walibaini kuwa mtuhumiwa Lucia Lukenya Mahizi hana mtoto aliyejifungua tarehe 17/04/2020. 

“Baada ya wananchi kubaini kuwa Lucia hana mtoto ndipo wananchi hao waliamua kutoa taarifa kwa jeshi la polisi na mtuhumiwa huyo alikamatwa siku hiyo ya tarehe 26/05/2020”,ameeleza Kamanda Magiligimba. 

Kamanda Magiligimba amesema chanzo cha mauaji hayo ni ugumu wa maisha baada ya kutelekezwa na aliyempa mimba. 

Kamanda huyo wa polisi amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mtuhumiwa alijifungua mtoto huyo tarehe 17/04/2020 na kumuua tarehe 19/04/2020 na kumzika mwenyewe pekee yake huko maeneo ya shule ya msingi ididi majira ya saa kumi na mbili na kasoro robo (11:45) jioni wakati mvua kubwa ikiendelea kunyesha ili watu wasimuone. 

“Mabaki ya mwili wa marehemu yalipatikana tarehe 26/05/2020 majira saa tisa alasiri katika kaburi alilozikwa na mtuhumiwa huyo na kukabidhiwa kwa ndugu kwa taratibu za mazishi”,ameongeza Kamanda Magiligimba. 

Kamanda Magiligimba anatoa wito kwa wananchi hususani wanawake kuacha kukatisha uhai wa watoto kwa sababu tu ya kutelekezwa na wenza wao bali wafike katika madawati jinsia na watoto yaliyopo vituo vya polisi na ofisi za ustawi wa jamii ili kupata ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527