MAHAKAMA KUU MUSOMA YASIKILIZA MASHAURI 18 KWA NJIA YA MAHAKAMA MTANDAO

Na. Francisca Swai- Mahakama Kuu Musoma
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, imesikiliza jumla ya mashauri kumi 18 kwa njia ya Mahakama Mtandao ‘Video Conference’ tangu ilipoanza kutumia teknolojia hiyo Mei 5, mwaka huu.


Akizungumzia matumizi ya Mahakama Mtandao, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe, John Kahyoza alisema walianza kusikiliza mashauri mawili yote yakiwa yanayohusu maombi ya kukata rufaa nje ya muda yalisikilizwa mbele yake wakati wafungwa wakiwa katika gereza la Musoma bila ya wao kufika Mahakamani.

Jaji Kahyoza alifafanua kuwa   mashauri 10 yalisikilizwa mbele yake, manne  yalisikilizwa na Mhe, Jaji, Zephrine Galeba  na mashauri yaliyobakia  yalisikilizwa na  Mhe, Jaji Ephery  Kisanya.

‘‘Mahakama ya Tanzania ilianza kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao muda mrefu katika baadhi ya Mahakama nchini ikiwa ni katika kutekeleza mpango mkakati wake wa miaka mitano (2015/2016 – 2019/2020). Hata hivyo jitihada hizo zimetiliwa mkazo kama njia ya kuepuka kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Corona vinavyosababisha homa ya mapafu (COVID 19)”, alisema Jaji Kahyoza.

Aliongeza kwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma pia imeanza kusikiliza mashauri kwa njia hiyo Mei 12, mwaka huu, ambapo mashauri matatu yalisikilizwa  mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe, Rahim Mushi na kuaihirishwa bila ya Wakili wa Serikali Mhe, Jesse Temba na washtakiwa kufika mahakamani hapo.

Jaji Kahyoza alisisitiza kwamba Mahakama hiyo, itaendelea kusikiliza mashauri kwa mtandao. Pia itawekeana ratiba maalumu na Mahakama ya Hakimu Mkazi, zikiwemo za Wilaya ili kutekeleza maagizo ya viongozi wa juu wa Mahakama wakiwemo viongozi wa kitaifa wanaosisistiza kuepuka msongamano na mikusanyiko hasa katika kipindi hiki cha janga la Corona.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post