ASKARI ALIYELAMBA CHEO KWA KUZAMA CHOONI KUOKOA MTOTO ATOA AHADI


Askari wa Zimamoto wilayani Ngara, Denice Minja.

Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilayani Ngara mkoani Kagera, Denice Minja ambaye alimwokoa mtoto katika shimo la choo cha shule ya msingi Murgwanza wilayani humo, ameahidi kumlea mtoto huyo katika maisha yake yote.

Akizungumza baada ya kuvishwa cheo kipya rasmi na Kamanda wa Zimamoto mkoa wa Kagera Hamis Dawa, askari huyo amesema kuwa amekwishafanya mazungumzo na mke wake na wote wamekubaliana kumlea, pia amefuatilia idara ya ustawi wa jamii na kuambiwa mtoto akiruhusiwa kutoka hospitali aende kwa ajili ya kupewa fomu ya kujaza ili akabidhiwe. 

Askari huyo amesema aliposikia sauti ya mtoto yeye kama mzazi alihisi uchungu na kuamua kujitoa mhanga kuingia katika shimo hilo lenye urefu wa mita 30 na baada ya kumfikia mtoto huyo mwenye jinsia ya kike alikuta amefungwa mdomo kwa khanga na kuwa hilo linathibitisha kuwa mhusika alilenga kumuua. 

Akimvisha cheo kipya cha Koplo kutoka cha zamani cha Konstebo, kamanda wa Zimamoto na Uokoaji mkoa wa mkoa wa Kagera, Inspekta Hamis Dawa amesema kuwa askari huyo amepandishwa rasmi cheo jana na Kamishna Jenerali wa jeshi hilo, John Masunga kutokana na ujasiri wake wa kuingia katika shimo kumwokoa mtoto huyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post