WAZIRI MKUU KUONGOZA MAOMBI YA KITAIFA KESHO JUMATANO VIWANJA VYA KARIMJEE DAR


Dodoma,  Jumanne 21 Aprili, 2020 
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Viongozi wa madhehebu ya Dini nchini, imeandaa maombi maalum Kitaifa kuiombea Nchi dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayotokana na Virusi vya Corona.


 Maombi hayo  yatakayoongozwa na Viongozi Wakuu wa  madhehebu ya Dini nchini, yatafanyika Jumatano tarehe 22 Aprili, 2020 katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam, kuanzia Saa 3.00 Asubuhi ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 Hatua hii ni utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa viongozi wa Dini na Serikali uliofanyika tarehe 9 Aprili, 2020 Jijini Dar es Salaam kuwa yafanyike maombi ya kitaifa yanayojumuisha madhehebu yote nchini kuomba dhidi maambukizi ya Corona.

 Aidha, maombi haya ni mwendelezo wa maombi ya siku tatu mfululizo yaliyotangazwa na Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kuanzia tarehe 17-19 Aprili, 2020.

 Viongozi wachache watahudhuria maombi haya kuwakilisha wananchi ikiwa ni katika hali ya kuchukua tahadhari ya maambukizi hivyo, wananchi mnasisitizwa kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Corona na kufuatilia maombi haya mkiwa katika maeneo yenu kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

JIKINGE, WAKINGE WENGINE CORONA INAZUILIKA.
 IMETOLEWA NA

   
Prudence Constantine,
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
(Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii).


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527