MWANDISHI MASHUHURI WA RIWAYA PROFESA KEN WALIBORA AFARIKI DUNIA….NI YULE ALIYESIFIKA KWA KITABU YA ‘SIKU NJEMA’


Riwaya ya Siku Njema ilitafsiriwa kwa Kiingereza na kuwa A Good Day
Mwandishi mashuhuri wa riwaya nchini Kenya, Profesa Ken Walibora amefariki dunia.

Prof Walibora aligongwa na gari katika barabara ya Landhies, jijini Nairobi Ijumaa na mwili wake umekuwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Taifa ya Kenyatta (KNH).

Alikuwa na miaka 55.

Kifo chake ni pigo kubwa kwa tasnia ya uandishi na kwa watetezi wa lugha ya Kiswahili.

Ingawa anakumbukwa sana kama mwandishi wa vitabu, amekuwa pia mtangazaji, mwandishi na msomi wa lugha ya Kiswahili.

Waliofanya kazi naye wanamwelezea kama mtu mnyenyekevu, mpenda watu na aliyekuwa na hamu sana ya kuwainua wengine na kuiendeleza lugha ya Kiswahili.

Rais Kenyatta ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu.

Amemsifu Prof Walibora kama mtangazaji na mwandishi vitabu aliyebobea na ambaye kazi zake za fasihi zitaendelea kuhamasisha vizazi na vizazi.

Siku Njema

Prof Walibora anafahamika sana kutokana na kitabu chake Siku Njema kilichochapishwa mwaka 1996. Ni kitabu ambacho Wakenya wengi walikisoma katika shule za upili kati ya 1997 na 2003. Kitabu hicho baadaye kilitafsiriwa kwa Kiingereza na kuwa A Good Day.

Kidagaa Kimemwozea pia ni kitabu kilichosomwa katika shule za upili.

Kwa jumla ameandika au kuchangia katika vitabu zaidi ya 40 kikiwemo Ndoto ya Almasi.

Prof Walibora alihariri au kuchangia katika vitabu vingi vya hadithi fupi na diwani za mashairi.

Aliandika pia vitabu vya watoto kama vile Ndoto ya Amerika kitabu ambacho kilishinda Tuzo ya Fasihi ya Jomo Kenyatta mwaka 2003.

Prof Walibora alisimulia kuhusu maisha yake ya utotoni kwenye tawasifu wake ya Nasikia Sauti ya Mama ambapo anaonesha maisha yake yalivyokumbwa na changamoto nyinyi zikiwamo maradhi,wivu na uadui kutoka kwa baadhi ya watu wa ukoo pamoja na umasikini miongoni mwa nyingine.

Katika tawasifu hiyo, anaeleza jinsi mamake alivyokuwa kichocheo kikubwa katika maisha yake ya utotoni. Anaeleza kuwa alikuwa ashiki na mchezaji wa kabumbu, mwanariadha na mchoraji.Tawasifu ya Naskia Sauti ya Mama pia ilishinda Tuzo ya Fasihi ya Jomo Kenyatta

Utotoni hadi kuwa msomi

Kennedy Walibora Waliaula alizaliwa mwaka 1964/65 katika eneo la Baraki, Bungoma magharibi mwa Kenya. Baadaye familia yake ilihamia eneo la Kitale na kisha Cherangany bado magharibi mwa Kenya. Baadaye alifupisha Kennedy na kuwa Ken.

Alifanya kazi kama mwalimu wa Kiswahili na Kiingereza katika shule ya upili kati ya 1985-86 kabla ya kuwa afisa wa kufuatilia watu waliofungwa vifungo vya nje katika wizara ya mambo ya ndani kati ya 1988 na 1996.

Alijitosa katika uanahabari baada ya hapo kwa kufanya kazi kama mtangazaji wa redio, mhariri na mtafsiri wa habari katika Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) hadi mwaka 1999 alipohamia shirika la habari la Nation Media Group na kuwa mtangazaji wa runinga na redio hadi 2004.

Wakati huo huo alikuwa akisomea shahada ya kwanza katika Fasihi na Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Nairobi ambapo alifuzu Mei 2004.

Kati ya 2005 na 2007 alikuwa mhariri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Ohio nchini Marekani ambapo alisoma shahada mbili za uzamili kwa wakati mmoja.

Alitawazwa profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison nchini Marekani mwaka 2009.

Baadaye alirejea katika kampuni ya Nation Media Group na kuwa mkuu wa ubora wa Kiswahili hadi mwaka 2017.

Hata baada ya kuondoka kwenye shirika hilo, amekuwa akichangia makala kwenye gazeti la Taifa Leo kwa jina Kauli ya Walibora.
Mlezi wa vipawa

Douglas Mutua, mwandishi na mwalimu wa Kiswahili Marekani, aliyewahi kufanya kazi na Prof Walibora, anasema atamkumbuka kama "mlezi wa vipawa".

Kishairi, ingawa alikuwa mwanamapokeo, kwa maana ya mshairi anayezingatia kanuni zote za ushairi, aliwatambua na kuwapa moyo walioandika mashairi huru.

Ni msomi asiyekubali usomi umwingie akilini na kumpokonya utangamano kati yake na watu.

"Ni mtu aliyeyachukua mashairi yangu nikiwa sina jina akayachapisha kwenye Diwani ya Karne Mpya. Kisha akafuatisha na mengine kwenye Diwani ya Waja-leo," anasema.

"Pia alikuwa mcheshi, mwadilifu na mnyenyekevu, mara nyingi akipiga gumzo na watu wa tabaka la chini kabisa. Si ajabu upate alikwenda kumzuru rafiki mkuu kwenye sekta ya Jua-Kali karibu na barabara ya Landhies alipogongewa na matatu."

Kutokana na uandishi wake wa kupigiwa mfano, aliwasadikisha wachapishaji wa vitabu kwamba mtu kutoka bara angeandika Kiswahili cha kufundishwa darasani.Kitabu cha Siku Njema kilitumiwa kufundishia fasihi kwa miaka mingi shule za upili Kenya

Ni kupitia uandishi wake mpevu, hasa wa riwaya ya Siku Njema, ambapo alichochea vipawa vya waandishi wengi kutoka bara wakajasiria kuandika.

Bw Mutua anasema marehemu alithamini sana vitu vitatu: Kiswahili, utu na soka.
CHANZO - BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post