RAIS KENYATTA ATANGAZA MARUFUKU YA KUINGIA NA KUTOKA NAIROBI,KILIFI,KWALE NA MOMBASA


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametangaza marufuku ya kuingia na kutoka katika kaunti za Nairobi, Kilifi, Kwale Mombasa huku idadi ya maambukizi ya virusi vya corona ikiongezeka kwa visa 16 zaidi.

Idadi ya watu walioambukizwa nchini Kenya sasa imefikia jumla ya watu 158 huku vifo vikiwa ni 6. Kwa mujibu wa rais Uhuru Kenyatta, watu 4277 wamefanyiwa vipimo vya virusi vya corona.

Bwana Kenyatta pia amewaagiza Wakenya wote kuvaa barakoa katika maeneo yote ya umma, na kuepuka maeneo yenye mikusanyiko ya watu ili kuepuka maambukizi ya virusi vya corona.

Marufuku ya kusafiri mjini Nairobi inaanza rasmi Jumatatu saa moja usiku kwa saa za Afrika Mashariki, huku marufuku hiyo kaunti za pwani, Kilifi, Kwale na Mombasa ikianza za Jumatano wiki hii ikitarajiwa kudumu kwa muda wa siku 21.

Hatua ya kuwekwa marufuku katika kaunti hizo nne, zimetokana na kaunti hizo kuwa na 96% ya visa vya virusi vya Corona nchini Kenya.

Asilimia 82 ya visa vya maambukizi ya corona viliripotiwa Katika jiji la Nairobi, huku asilimia 14 ya visa hivyo katikana katika kaunti za pwani ya Kenya za Kilifi, kwale na Mombasa

Marufuku hiyo imewekwa dhidi ya safari zote za majini, angani na nchi kavu ili kuzuia maambukizi ya corona yanayoongezeka kwa kasi nchini Kenya na maeneo mengine duniani.

Marufuku hii imetangazwa na rais Kenyatta huku Wakenya wakiendelea kutekeleza amri ya kutotoka nje kuanzia saa moja za jioni hadi saa kumi na moja asubuhi iliyotangazwa wiki iliyopita, lakini kulingana na Mkuu wa wafanyakazi katika ikulu ya rais Kenyatta, matembezi ndani ya jiji la Nairobi yataendela kwa kuzingatia sheria iliyowekwa ya marufuku hiyo.
Rais Kenyatta amesema huku janga na corona likiendelea kuikumba Kenya na mataifa mengine duniani, Wakenya wanapaswa kubadili tabia kwa kunawa mikono na kutosogeleana.

Amesema iwapo janga hili litaendelea kusababisha maafa zaidi Wakenya wajiandae kwa hatua zaidi za kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.



Uhuru Kenyatta amewataka Wakenya kuzingatia hatua zifuatazo :
Kuvaa barakoa kila mara wanapokua katika maeneo ya umma
Kunawa mikono kwa sabuni.


Kuendelea kuepuka kukaribiana na kuzingatia ushauri wa kukaa mita mbili kutoka kwa mtu mwingine.


Wasiwaweke hatarini watu wenye umri wa zaidi ya miaka 50 na wenye magonjwa ya kudumu.


Amewataka mafundi wa nguo kutengeneza barakoa nyingi na akasema maafisa wa afya watawaelekeza namna zinavyotengenezwa.


Gari lolote la mizigo halitaruhusiwa kuwa na watu zaidi ya watatu na inapaswa kuwa na kibali cha maafisa
Usafirishaji wa chakula utaendelea kama kawaida
H
atua za awali:


Wiki iliyopita wizara ya afya nchini humo ilitangaza wazi kuwa kwamba inatengeneza barakoa ambazo zitasambazwa kwa wananchi hivi karibuni.

Wizara ya afya imeeleza kuwa watu watakaokufa kutokana na virusi vya Corona watazikwa ndani ya saa 24 huku watu wa karibu wa familia wasiozidi 15 wakiruhusiwa kuhudhuria mazishi hayo yatakayoandaliwa na Serikali.

Aidha, ndege kutoka nchi za kigeni zimeendelea kipigwa marufuku kuingia Kenya kwa siku 30 zaidi.

Hatahivyo, marufuku hii iliondolewa kwa ndege za kigeni zinazokuja kuhamisha raia wa nchi za nje waliokwama ingawa zinatakiwa kutoa taarifa kwa serikali angalau saa 72 kabla.

Ndege zingine ambazo hazitaathirika na marufuku hii ni zile za kubeba mizigo hasa ikizingatiwa kwamba kwa sasa serikali inaagiza vifaa vya wahudumu wa afya kutoka nje.

Na kutokana na ongezeko hilo, kuanzia Jumatatu, matatu au daladala pamoja na bodaboda ambazo zitakiuka sheria zilizowekwa zitapokonywa leseni na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kusambaza virusi kimaksudi.
Chanzo- BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527