CAG ASEMA MALIASILI WAMETUMIA BIL 2 KINYUME CHA UTARATIBU, KIGWANGALLA AFUNGUKA


Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Tanzania (CAG) imebaini matumizi ya Sh2.58 bilioni yaliyofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii nje ya bajeti na kabla ya kupitishwa na Bunge.Hayo yamebainishwa katika ripoti kuu ya mwaka kuhusu ukaguzi wa taarifa za fedha za serikali kuu kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2019. Fedha hizo zimetumika kufanikisha kampeni ya Urithi Festival Celebration and Channel maalum ya kutangaza vivutio vya utalii kinyume na taratibu.

“Nilipitia matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii na kubaini kiasi cha Sh 2.58 bilioni kimetumika kuanzisha chaneli ya Televisioni “Urithi Festival” ili kutangaza vivutio vya utalii,” imeeleza ripoti hiyo.


Imeeleza kuwa katika kutambua chanzo ya kugharamia matumizi hayo, hayakuwa na kifungu cha bajeti kama ilivyopitishwa na Bunge.

Imeeleza kuwa fedha hizo zilitolewa katika vifungu vingine vya matumizi ya wizara na taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo ambazo ni Tanapa, NCAA, Tawa na TFSA.

“Nilijulishwa kuwa bajeti ya Urithi Festival ilipitishwa na menejimenti ya Wizara katika vikao mbalimbali vilivyofanyika,” inaeleza taarifa hiyo.

Akinukuu Ripoti ya CAG, Mbunge wa Viti Maalum Chadema, Catherine Ruge, amesema kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii nchini Tanzania ilitumia TZS 2.5 bilioni kuanzisha Channel ya runinga-Urithi Festival nje ya Bajeti iliyopitishwa na Bunge.

Naye Waziri Maliasili, Dkt. Hamisi Kigwangalla, amesema; “Mimi siyo mwizi, siibagi, na sichukuagi rushwa. Kwenye maeneo ambayo mtu yeyote anayenitafuta kuniharibia hadhi na heshima yangu kama kiongozi msafi huwa mara zote anakwama ni hapo kwenye tamaa ya pesa ya umma. Huwa sina. Hivyo hii vita ni rahisi sana kwangu.

“Ukitaka kunichafua mimi, tafuta kasoro zangu zingine, lakini hautonipata kwenye rushwa, uonevu, dhulma, wizi, matumizi mabaya ya ofisi, uzembe, uvivu wala ujinga/upuuzi. Nitafute kwingine. Nitatoa ufafanuzi juu ya utaratibu baada ya masaa matatu,” amesema Waziri Maliasili, Dkt. Hamis Kigwangalla.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post