ASKOFU MWAKIPESILE AWATAKA WANANCHI KUENDELEA KUTII MAELEKEZO YANAYOTOLEWA KUHUSU CORONA BADALA YA KUBEZA


Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Dkt. Brown Mwakipesile
***
Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Dkt. Brown Mwakipesile ameiasa jamii kuendeleea kutii maelekezo yanayotolewa na Serikali ili kuendelea kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona na kuhakikisha nchi inakuwa salama na kuondokana watu wanaopuuza maelekezo yanayotolewa.

Ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ibada ya jumapili (5 Aprili, 2020) katika kanisa la EAGT Mlimwa West Jijini Dodoma kuhusu uwepo wa ugonjwa huo na namna Kanisa lilivyopokea maelekezo yanayoendelea kutolewa na Serikali na kuyaishi kwa vitendo.

Dkt. Mwakipesile alieleza kuwa kila Mtanzania ananafasi ya kujali maelekezo muhimu ya kuzingatia wakati wa janga hili la corona na kuwa watii ili kuendelea kupambana na ugonjwa huu na kuhakikisha kila mmoja anakuwa balozi mwema kwa kupambana na janga lililopo nchini.

Aidha alieleza kuwa, majanga yanapotokea ni muhimu kuwa na utulivu na tafakari juu ya hali iliyopo na kuangalia namna bora ya kuenenda na kukubali uwepo wa Mungu katika maisha ya kila mwandamu ili aweze kuponya na kuweka nchi katika hali ya usalama.

“Usalama wa kila mwanadamu upo katika mikono ya Mungu hivyo majanga yanapotokea hatuna budi kuwa watii katika maelekezo yanayopaswa kufuatwa na kuendelea kumgeukia Mungu katika changamoto hii ya corona,”Alieleza

Mwakipesile alieleza kila mmoja ahakikishe anaiombea nchi kwa bidii na kuipenda kwa kuwa Mungu alituweka ndani ya nchi hii kwa makusudi ili kuwa waombezi na walinzi wa nchi yetu wenyewe.

Alifafanua kuwa, ni wakati sahihi wa kuendelea kuunga mkono kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ya kuamini Mungu pekee ndiye mwenye Mamlaka na uweza wa kuponya na kuokoa nchi ya Tanzania ikiwa ni sambamba na kuruhusu Watanzania kuendelea kufanya ibada huku wakifuata miongozo na melekezo yanayotolewa na Serikali.

Sambamba na hilo ameendelea kupongeza viongozi wa dini kwa mwitikio chanya wa kutii na kuweka taratibu za kujikinga na maambukizi ya virusi hivi kwa kuwahimiza waumini wao kunaa mikono kila wakati, matumizi sahihi ya sanitizer, kuhakikisha wanapokuwa ndani ya nyumba za ibada wanakaa umbali wa mita kati mtu mmoja na mwingine ili kuzuia maambukizi hao.

“Kipekee ninampongeza Mkuu wa Nchi yetu kwa kuona umuhimu wa kuruhusu Wananchi kumwabudu Mungu na kuomba kwa bidii, hii ni ishara tosha kuwa Tanzania itaendelea kuwa salama kwa kuzingatia nguvu iliyopo katika maombi na uhakika wa uponyaji wa Mungu nchini,”alisema Dkt. Mwakipesile

Dkt. Mwakipesile alieleza miongoni mwa sababu zinazoruhusu uharibifu ndani ya Taifa ni endapo watu wakashindwa kujizui kutenda dhambi na kugeukia mambo maovu na kuruhusu nguvu za shetani kutesa watu badala ya kumruhusu Mungu kutawala na kuendelea kuponya nchi yao.

“Lazima ifahamike kuwa, nchi itakuwa huru na mahali salama endapo watu wake wataendelea kumgeukia Mungu na kuachana na matendo maovu katikati yao naye Mungu ameahidi kuliangalia Taifa la jinsi hiyo na kuponya uharibifu wa kila aina ikiwemo magonjwa,”alisema Dkt. Mwakipesile

Aidha Dkt. Mwakipesile alitumia fursa hiyo kuwaasa viongozi wote wa dini kuendelea kutii Mamlaka zilizopo kwa kuwa zimewekwa na Mungu Dunia na kuwataka Watanzania kuendelea kutambua na kuunga mkono jitihada za viongozi wetu kwa matendo.

“Rais wetu amekuwa wa kipekee na mfano kwa kutambua uwepo wa Mungu na ni lazima tumuombee sana pamoja na viongozi wote na kuzingatia uwepo wetu Tanzania ni kwa makusudi kaisa pasipo kubeza hilo,”alisema

Sambamba na hilo aliwatoa hofu wananchi wote kwa kuzingatia maombi yanayoendelea nchini kuhusu ugonjwa huo na kueleza ni wakati pekee wa kujitenga na dhambi na uovu wa kila namna kisha kumgeukia Mungu pekee ili kupata rehema na haki ya kuponywa.

“Jambo la Msingi katika maisha ya mwanadamu aendelee kutambua nafasi ya Mungu kwa maana ukiacha kumhofu Mungu unapoteza haki ya kupokea uponyaji wake na kubaki katika mateso ambayo hayakuwa mpango wa Mungu kwa wanadamu,”alisisitiza Dkt. Mwakipesile.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527