ZITTO KABWE ATAJA MAMBO 8 KUKABILIANA NA CORONA


Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ametoa mapendekezo manane kupitia barua aliyomwandikia Rais John Magufuli, kuhusu nini kifanyike katika kuzuia maambukizi mapya ya ugonjwa wa corona.


Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini, kwenye barua hiyo alitoa pia ushauri juu ya namna nzuri ya udhibiti wa maambukizi ya ugonjwa huo, ambao umekuwa tishio katika nchi nyingi duniani.

Kwanza, Zitto alipendekeza kuwapo kwa umoja wa kitaifa ambao utawaweka Watanzania pamoja kwa vitendo hali itakayofanikisha kupambana na ugonjwa huo.

“Hakuna wakati nchi yetu inahitaji umoja kama wakati huu. Wewe kama mkuu wa nchi una wajibu mkubwa wa kuwaweka Watanzania pamoja kwa vitendo. Tukiwa wamoja tutaweza kupambana na corona na kushinda pamoja na ikibidi kushindwa tushindwe pamoja,” alisema Zitto na kuongeza:

“Corona haitambui itikadi zetu za vyama, dini zetu wala makabila yetu. Corona inaua mashekhe na makasisi, wanasiasa na wananchi wa kawaida, wanadiplomasia na wanamichezo na mbaya zaidi inaua hata wataalamu wa afya kama madaktari na manesi. Nakusihi sana, uunganisha nchi yetu sasa bila kuchelewa,” alisema Zitto.

Pili, Zitto alipendekeza wataalamu kupewa nafasi katika kuongoza mapambano na kwamba viongozi kuepuka kutoa maeneo ya jumla.

“Ni muhimu sana sisi viongozi kuepuka kutoa maneno ya jumla ambayo yanawapa wananchi wetu matumaini hewa, hivyo kusababisha hatari zaidi. 

“Tutoe nafasi kwa wataalamu wa afya kutuongoza katika mapambano haya ya kudhibiti corona. Ni lazima sasa, maneno tunayoyasema kwa umma na maamuzi tunayoyachukua katika kudhibiti mlipuko huu yazingatie ushauri wa wataalamu ,” alisema Zitto.

Tatu, alipendekeza serikali kuweka nguvu kubwa kwenye kupima wananchi ili kuwatambua wenye maambukizi, kuwatenga wasiambukize wengine, kuwatibu na kuwafutilia maendeleo yao.

Zitto alisema kazi ya upimaji iwe kampeni endelevu na kwamba serikali itumie vipimo ilivyosaidiwa sambamba na kutumia fedha za dharura ambazo Bunge lilizipitisha kwenye bajeti ya mwaka 2019/2020 kununua vipimo vingi zaidi ili kupima wananchi.

Nne, Zitto alipendekeza kuwapo na uwazi wa takwimu za maambukizi mapya, wagonjwa mahututi na vifo kwani suala hilo ni muhimu sana katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Tano, Zitto alipendekeza kuepukwe maelekezo yanayopinga na kueleza kuwa hatua zichukuliwe kusimamisha vikao vyote vya kiserikali ikiwamo Bunge na Mahakama.

“Serikali ilichukua hatua muafaka kufunga shule na vyuo kote nchini ili kuzuia maambukizi. Hata hivyo, tunatuma ujumbe gani kwa wananchi, na hasa watoto wetu wanapoona wao wamefunga shule, lakini viongozi wanahutubia makumi ya watu hadharani? Wanapata ujumbe gani wanapoona Bunge linaendelea na vikao?” Alisema Zitto.

Sita, alipendekeza mahabusi na wafungwa waachiliwe na warudi nyumbani ama kumalizia vifungo au kusubiri upelelezi wa kesi zao.

Saba, Zitto alipendekekeza kufungwa kwa mipaka ya nchi kwa muda ili kudhibiti maambukizi, na kwamba kwa kufanya hivyo kutasaidia kuzuia maambukizi zaidi.

“Ni lazima kuzuia msongamano wa watu kwenye huduma za usafiri wa umma kwa kuagiza vyombo vya usafiri vya Jeshi la Wananchi, Polisi na hata watu binafsi kutoa huduma ya usafiri wa umma kwa uangalifu mkubwa,” alisema Zitto.

Nane, Zitto alipendekeza kuundwa kwa timu ya wachumi waliobobea waliopo ndani na nje ya serikali watakaofanya uchambuzi wa kina wa hali ya uchumi wa nchi na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post