WAISRAELI WAPIGA KURA TENA LEO ... HATMA YA WAZIRI MKUU NETANYAHU KUJULIKANA USIKU WA MANANE


Wananchi wa Israeli wanapiga kura leo Jumatatu katika uchaguzi usio wa kawaida na wa tatu nchini humo katika kipindi cha mwaka mmoja. Uchaguzi huu ndio utaamua kujulikana hatma ya Waziri Mkuu wa Benjamin Netanyahu ambaye anakabiliwa na kesi ya mashitaka ya ufisadi.

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa saa moja asubuhi na vitafungwa saa nne kamili usiku. Matokeo rasmi yanatarajiwa usiku wa manane.

Benjamin Netanyahu anakabiliwa na ushindani mkali kwa mara nyingine kutoka kwa jenerali mstaafu wa jeshi Benny Gantz, ambaye chama chake cha Bluu na Nyeupe au Blue and White, kinapambana kwa nguvu sawa na cha Netanyahu Likud kikituma ujumbe kuwa waziri mkuu huyo wa muda mrefu wa Israel hastahili kuongoza kwa sababu ya mashitaka makubwa dhidi yake.

Israel imeweka vituo 15 kuruhusu upigaji kura wa mamia ya Waisrael walioamrishwa kubaki majumbani mwao baada ya kuwa katika kitisho cha kuambukizwa virusi vya corona.

Hata hivyo mwanasiasa mashuhuri Avigdor Lieberman ameahidi kuwa hakutakuwa na uchaguzi wa nne.

Lieberman hajatangaza anamuunga mkono mgombea yupi, ijapokuwa Netanyahu au Gantz hawatapata wingi wa viti bungeni bila msaada wake.

Netanyahu anatarajia kufikishwa mahakamani Machi 17 kwa mashitaka ya ufisadi, ulaghai na uvunjifu wa uaminifu kutokana na tuhuma kuwa alikubali zawadi za kifahari kutoka kwa marafiki wake mabilionea.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post