Picha : KAMATI YA USHAURI YA WATU WENYE ULEMAVU SHINYANGA YAKUTANA KUJADILI NA KUTATUA CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILIKamati ya ushauri ya watu wenye ulemavu mbalimbali mkoa wa Shinyanga imefanya kikao kwa mara ya kwanza, ili kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabiliwa watu wenye ulemavu mbalimbali likiwamo suala la ajira na mikopo ili kuwainua kiuchumi.


Kikao hicho kimefanyika leo, Machi 12,2020 katika hospitali ya rufani ya mkoa wa Shinyanga ambapo mgeni rasmi alikuwa kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt. Nuru Mpuya.

Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho, Dkt. Mpuya, alisema kikao hicho ni fursa ya kujadili changamoto ambazo zinawakabili watu wenye ulemavu, ili kuona namna ya kuzitatua ili kuboresha huduma na maslahi ya watu wenye ulemavu mkoani Shinyanga.

“Kikao hiki cha kamati ya ushauri ya watu wenye ulemavu mkoa wa Shinyanga, ni fursa tosha kwenu kujadili yale ambayo Serikali imewatendea pamoja na changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi. Siku zote msitegemee mtu kutoka nje kuja kuwasemea matatizo yenu bali ni nyinyi wenyewe,” alisema Dk. Mpuya.

Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu Tanzania mkoa wa Shinyanga (SHIVYAWATA), Richard Mpongo, ameipongeza Serikali kuunda Kamati hiyo ya ushauri kwa watu wenye ulemavu mkoa, ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu.

Aidha alisema changamoto kubwa inayowakabili watu wenye ulemavu mkoani Shinyanga ni taasisi binafsi pamoja na viwanda kushindwa kuzingatia Sheria ya kuajiri watu wenye ulemavu, kama inavyofanya Serikali.

“Tunaomba taasisi hizi binafsi pamoja na viwanda, vipatiwe elimu juu ya kuzingatia Sheria ya watu wenye ulemavu, ambayo inataka asilimia tatu ya waajiriwa wawe walemavu, lakini imekuwa haizingatiwi na sisi kuendelea kuishi maisha magumu, licha ya kuwa na sifa za kuajiriwa,”alisema Mpongo.

“Serikali haina Shida juu ya kuajiri watu wenye ulemavu, mfano huko wilaya ya Kishapu kuna afisa mtendaji kijiji cha Mwamadulu ni mlemavu wa macho, na alifanya usahili mwaka 2018 na sasa anafanya kazi vizuri tu ya kuhudumia wananchi, hivyo taasisi hizi binafsi zitupe fursa,”aliongeza.

Naye Afisa ustawi wa jamii mkoa wa Shinyanga Lidya Kwesigabo, alisema tatizo hilo hata Serikali wameshaliona, na ndiyo maana wameitisha kikao hicho cha watu wenye ulemavu, ili wapange mikakati ya kuanza kutembelea taasisi hizo binafsi pamoja na viwanda, kutoa elimu ya kuajiri watu wenye ulemavu.


TAZAMA PICHA HAPA CHINI

Kaimu Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt. Nuru Mpuya, akizungumza kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya watu wenye ulemavu mkoa wa Shinyanga leo Alhamis Machi 12,2020. Picha zote na Marco Maduhu - Malunde 1 blog

Afisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Shinyanga Lidya Kwesigabo, akizungumza kwenye kikao hicho cha kamati ya ushauri ya watu wenye ulemavu mkoa wa Shinyanga.

Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Richard Mpongo, akizungumza kwenye kikao hicho cha kamati ya ushauri ya watu wenye ulemavu mkoani Shinyanga.

Mwenyekiti wa chama cha magonjwa yasiyo yakuambukiza Kanda ya Ziwa Ruth Kanoni, akitoa elimu kwenye kikao hicho namna ya kujikinga na maambukizi dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kikiwamo kisukari na Shinikizo la damu.

Kushoto ni Afisa afya kutoka ofisi ya mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mussa Makungu, akitoa elimu ya Virusi vya Corona kwenye kikao hicho, na kutaja dalili za ugojwa huo wa Corona, kuwa ni kukohoa mara kwa mara, kupumua kwa shida sababu ya kuathiri kwenye mapafu, homa kali, na kutaja kinga yake ni kunawa mikono na kutoshikana, kupiga chafya kwa kujifunika na kitambaa, huku akiwataka wananchi wakimuona mtu ana dalili hizo watoe taarifa kwenye huduma za afya.

Kushoto ni Afisa afya kutoka ofisi ya mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mussa Makungu, akielezea maeneo ambayo Serikali imeshayatenga kwa ajili ya wagonjwa wa virusi vya Corona, kuwa Shinyanga manispaa kituo cha afya Kambarage, Ushetu kituo cha afya Bulungwa, Msalala kituo cha afya Bugharama, Shinyanga vijijini kituo cha afya Tinde, Kahama kituo cha afya Mwendakulima, pamoja na Kishapu kituo cha afya Kishapu.

Wajumbe wakiendelea na kikao.

Wajumbe wakiendelea na kikao.

Wajumbe wakiendelea na kikao.

Mjumbe Mohamed Ally akichangia mada kwenye kikao hicho.

Mjumbe Justine Shindayi akichangia mada kwenye kikao hicho.

Wajumbe wakipiga picha ya pamoja mara baada ya kumaliza kikao.

Picha zote na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post