TAASISI WIZARA YA KILIMO ZATAKIWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE KWA WELEDI

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Taasisi zilizopo Wizara ya Kilimo pamoja na Bodi za Mazao zimetakiwa kufanya kazi kwa Bidii na utashi mkubwa ili kutekeleza matakwa na taswira ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Ndg Gerald Kusaya ameyasema hayo jana Tarehe 11 Machi 2020 wakati akizungumza na Uongozi na watumishi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) katika ofisi za makao makuu ya Taasisi hiyo eneo la Makutupora Jijini Dodoma.

Kusaya amesisitiza kuwa wataalamu hao wanapaswa kufanya Utafiti na kuonyesha matokeo chanya ya utafiti huo, Ameongeza kuwa utafiti haupaswi kuishia kwenye makaratasi pekee bali matokeo chanya kwa wakulima.

Amesema kuwa Wizara ya Kilimo inashika nafasi ya pili kwa kuwa na wasomi wengi kwa ngazi za PHD na Maprofesa hivyo taaluma hiyo inapaswa kuwa na matokeo chanya kwani kutokuwa na matokeo hayo ni kazi bure kwa wananchi na uwepo wa taasisi hiyo.

Kuhusu Changamoto ya fedha kwa ajili ya utafiti wa Mazao iliyobainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Dkt Geoffrey Mkamilo, Katibu Mkuu huyo amesema kuwa hakuna mafanikio ya kilimo bila kuimarisha utafiti hivyo lazima kutafuta njia ya kupata fedha kwa haraka ili kuendeleza utafiti.

Kusaya ametoa mwito kwa wafanyakazi wa TARI kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kujiendeleza kielimu. "Taasisi ya utafiti ni muhimu sana kwa watu kujielimisha zaidi, Hata kama una miaka 60 sisi tutakupeleka shule, hakuna kada ambayo tutaiacha zote tutazipeleka shule ili tuweze kwenda na wakati" Alikaririwa Katibu Mkuu Ndg Kusaya

Hii ni ziara ya kwanza ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Ndg Gerald Kusaya tangu alipokabidhiwa kijiti kuiongoza wizara hiyo kama mtendaji Mkuu Machi 6, 2020.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post