MBWANA SAMATTA APANIA KUWEKA HISTORIA LEO UWANJA WA WEMBLEY


Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Mbwana Samatta, ambaye anakipiga katika klabu ya Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu nchini England, leo atakuwa kwenye Uwanja wa Wembley kukipiga dhidi ya Manchester City.

Samatta ataongoza safu ya ushambuliaji ya Aston Villa kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Carabao dhidi ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu nchini England.

Hii ni mara ya kwanza kwa mchezaji wa kitanzania kucheza michuano hiyo ya Carabao pamoja na kucheza fainali kwenye uwanja huo wenye historia kubwa nchini England.

Samatta alijiunga na Aston Villa wakati wa uhamisho wa dirisha dogo la usajili la Januari mwaka huu akitokea katika klabu ya KRC Genk ya nchini Ubelgiji baada ya kuonesha kiwango cha hali ya juu kwa kipindi cha misimu minne.

Hadi sasa tangu asajiliwe, amefanikiwa kucheza jumla ya michezo mitatu ya Ligi Kuu nchini Uingereza na kufanikiwa kupachika bao moja kwenye mchezo dhidi ya Bournemouth, huku Aston Villa wakipigwa mabao 2-1.

Samatta amedai kucheza kwenye Uwanja wa Wembley dhidi ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England kwake ni kama ndoto, hivyo lazima apambane ili kuiandikia historia klabu yake na yeye mwenyewe kwa ujumla.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527