WAKUU WA WILAYA, WAKURUGENZI WAPEWA AGIZO ZITO WANAFUNZI WANAOZAGAA HOVYO ...CORONA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo ameagiza Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi na Wakuu wa shule nchini, kuhakikisha wanasafirisha wanafunzi waliokosa usafiri badala ya kuwaacha wakizagaa hovyo.

Machi 17, mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifunga shule zote za msingi na sekondari kwa siku 30 kutokana na tishio la ugonjwa wa Corona.

Agizo hilo amelitoa leo Machi 20, 2020 wakati akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dodoma. 

Amesema baadhi ya mikoa wanafunzi wameonekana kuzagaa na wengine kulala kwenye vituo vya mabasi kutokana na viongozi hao kutotekeleza agizo la kuhakikisha wanasafiri kwa usalama na amani hadi makwao.

"Kama kuna shida wakuu wa shule wawasiliane na wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama ambao ni wakuu wa wilaya, haileti picha nzuri kuona wanafunzi wamezagaa vituoni wakitafuta usafiri jambo ambalo linadhihirisha kuwa wakuu wa shule hawakujipanga vizuri," amesema.

Ametoa pongezi kwa Mkuu wa Shule ya Kilakala iliyopo Morogoro na Mkuu wa Shule ya Dodoma Sekondari kwa kuweka utaratibu mzuri wa kusafirisha wanafunzi hao.
CHANZO- NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527