JIKO LA MKAA LAUA BABA,MAMA NA WATOTO WAKIJIKINGA NA BARIDI YA MVUA KAHAMA



Nyumba ambayo marehemu walikuwa wamelala

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Watu wanne wa familia moja wamefariki dunia baada ya kuvuta ya hewa yenye sumu ya Carbon monoxide iliyotokana na mkaa waliowasha kwenye jiko la mkaa kisha kulala ndani ya nyumba yao wakijikinga na baridi iliyotokana na mvua kubwa katika kitongoji cha Ngilimba ‘B’ kijiji cha Ngilimba kata ya Ulowa halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga. 


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Machi 28,2020 ambapo ndugu hao wa familia moja waligundulika kuwa wamefariki dunia wakiwa nyumbani kwao wamelala baada ya kuvuta hewa yenye sumu ya Carbon Monoxide. 

“Chanzo cha tukio hilo ni kwamba siku hiyo mvua kubwa ilinyesha kijijini hapo na kupelekea uwepo wa baridi nyumbani kwa marehemu hao na ndipo wakati wakijiandaa kulala waliacha jiko la mkaa likiwa limewashwa ndani ya nyumba na kufunga mlango na dirisha hali iliyopelekea mgandamizo wa hewa kuwa mdogo ndani ya nyumba yao na kuvuta hewa hiyo iliyokuwa na sumu ya carbon monoxide”,amesema Kamanda Magiligimba. 

“Waliofariki dunia ni Masanja Emmanuel (35) ambaye ni baba wa familia hiyo  na mkewe Mngole Masanja (25), Holo Masanja,(05) na Matama Masanja (03) wote wakazi wa Ngilimba wote wa familia moja”,ameeleza Kamanda Magiligimba 

Amesema miili ya marehemu imekabidhiwa ndugu kwa ajili ya mazishi baada ya kufanyiwa uchunguzi wa daktari.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527