ALIYEUA NA KUTOKOMEA NA KICHWA CHA MAREHEMU AUAWA AKIJARIBU KUWAKIMBIA POLISI...MAMA NAYE AUA MTOTO ILI AOLEWE


Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza ndani ya wiki hii llifanikiwa kumkamata mtuhumiwa aliyetenda kosa la mauaji , kutoroka na baadae kukificha kichwa cha marehemu kusikojulikana baada ya kukikata , pia linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wao kwa madai ya kuimarisha mahusiano ya kimapenzi.


Tukio la kwanza.
Tarehe 09/03/2020 majira ya 08:05hrs huko maeneo ya msitu wa Machemba, kata ya Isamilo, wilaya ya Nyamagani, jiji na mkoa wa Mwanza, mtoto wa mtaani asiyefahamika utambulisho wake, jinsia ya kiume, anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 15 -20, alikutwa akiwa ameuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali hadi kutenganisha kichwa na kiwili wili na mtu ambaye baada ya uchunguzi alifahamika kwa jina la Abdul Rahaman Abdalah, miaka kati ya 25-30, Mzaramo, mkazi wa Mabatini, jijini Mwanza. 

Mtuhumiwa huyo baada ya kutenda kosa hilo la mauaji aliondoka na kichwa cha marehemu na alipokamatwa alidai angekipeleka kwa mganga wa kienyeji.

Ufuatiliaji wa polisi ulifanikisha kumtia mbaroni mtuhumiwa tarehe 12.03.2020 na baada kuhojiwa kwa kina alikiri kuhusika na mauaji hayo na alikubali kwenda kuwaonesha askari sehemu alipokua ameficha kichwa cha Marehemu huko katika mlima wa Machemba uliopo wilaya ya Nyamagana. 

Na baada ya kufika eneo hilo akiwa na makachero wa polisi mtuhumiwa alichimba ardhini na kutoa kichwa cha marehemu ambacho alikua amekifukia na ghafla aliwarushia askari kichwa hicho na kuanza kukimbia, ndipo askari walilazimika kufyatua risasi nne hewani na kumuamuru kusimama lakini alikaidi na baadae askari walifyatua risasi tatu wakati akikimbilia Mlimani na zilimpata miguuni na maeneo ya paja na mgongo akakamatwa lakini alifariki dunia akiwa njiani wakati anakimbizwa kupelekwa hospitali ya rufaa ya mkoa Sekou Toure Mwanza .

Miili ya marehemu wote wawili imehifadhiwa hospitali ya rufaa ya mkoa Sekou Toure kwa ajili ya uchunguzi na utambuzi, pindi uchunguzi uunaendelea kujua chanzo cha mauaji ya awali

Tukio la pili;
Tarehe 12.03.2020 majira ya 19:00hrs huko kitongoji cha Mwashega, kijiji cha Bugembe kata na tarafa ya Nyamilama, wilaya ya Kwimba, iligundulika kuuawa kwa mtoto aitwaye Abdallah James Simon, umri wa miezi 9, kwa kunyongwa kwa kutumia kamba na mama yake mzazi aitwaye Helena Nestory Washera, miaka 19, msukuma, mkazi wa kijiji cha Bugembe kwa kushirikiana na mpenzi wake aitwaye Lucas Jackson @ Kajanja, miaka 24, msukuma, mkazi wa kijiji cha Bugembe, kisha kuutupa mwili wa mtoto huyo vichakani, kitendo ambacho ni kosa la jinai.

Mauaji hayo yalitokea tarehe 25.02.2020, hii ni baada ya mama wa mtoto kuelezwa na mpenzi wake wa sasa aitwaye Lucas Jackson kuwa amuue mtoto wake huyo ili aweze kumuoa. 

Inadaiwa kuwa baada ya mwanamke huyo kuelezwa hivyo ndipo wote kwa pamoja walifanya uhalifu huo na kuendelea na mahusiano yao ya kimapenzi.

Hata hivyo baada ya muda kupita , baba mzazi wa mtoto aitwaye James Simoni alikwenda kumsalimia mwanae na kuambiwa na mzazi mwenzake kuwa mtoto yupo kwa bibi yake na baadae alifanya ufuatiliaji lakini alimkosa ndipo alitoa taarifa polisi. 

Jeshi la polisi lilifanya ufuatiliaji na kuweza kuwakamata watuhumwa hao na baada ya kuhojiwa kwa kina walikiri kuhusika na mauaji hayo na kwenda kuonesha sehemu walipotupa Mwili wa mtoto huyo, ambapo katika eneo la tukio ilikutwa mifupa inayosadikiwa kuwa mabaki ya mwili wa mtoto mdogo. Mabaki hayo yamepelekwa kwa mkemia mkuu wa serikali kwa ajili ya uchunguzi.

Jeshi la polisi mkoa wa mwanza linatoa wito kwa viongozi wa dini, viongozi wa taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za serikali kuendelea kuwaelimisha wananchi kuacha tabia ovu kama hizi ambazo ni kinyume na sheria za nchi na maadili ya mtanzania. 

Vilevile linaendelea kuwasihi wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuzuia kutendeka kwa kukamatwa na kufikishwa katika vyombo Vya sheria.

 IMETOLEWA NA;
Muliro J. MULIRO – ACP.
KAMANDA WA POLISI (M) MWANZA
14 MARCH, 2020


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527