TANZANIA KUSHIRIKIANA NA UJERUMANI KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI SEKTA YA UHIFADHI WA MALIASILIA NCHINI

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Ujerumani katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya uhifadhi wa maliasili hapa nchini kwa lengo la kuiimarisha na kuiendeleza sekta hiyo.


Dkt. Kigwangalla ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya uhifadhi inayofadhiliwa na serikali ya Ujerumani katika Hifadhi ya Taifa Nyerere - Selous.

Akiwa ameambatana na Mwakilishi wa Kansela wa Ujerumani, G√ľnter Nooke na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzani Regine Hess, Waziri Kigwangalla ameishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za uhifadhi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania.

Dkt. Kigwangalla amesema kuwa Ujerumani kupitia taasisi zake na mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali yakiwemo ya GIZ , KFW na Frankfurt Zoological Society (FZS) yamekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza shughuli za uhifadhi wa maliasili hapa nchini kwa kushirikiana na taasisi za uhifadhi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii akibainisha kwamba Sensa ya Tembo na Wanyamapori wengine wakubwa ya mwaka 2018 iliyofanyika katika Ikolojia ya Nyerere - Selous - Mikumi ni moja ya matokeo ya ushirikiano huo.

Kwa upande wake Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Regine Hess ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa juhudi kubwa inazofanya za kuimarisha ulinzi wa maliasili na kudhibiti vitendo vya ujangili.

Amesema kuwa kuimarika kwa shughuli za uhifadhi nchini Tanzania ni matokeo ya ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi ya Tanzania na Ujerumani na kuongeza kuwa Ujerumani itaendelea kusaidia na kuunga mkono juhudi za uhifadhi nchini Tanzania kupitia programu na miradi mbalimbali.

Ziara hiyo pamoja na kujikita katika kuangalia miradi ya uhifadhi inayofanywa na Ujerumani katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere pia imeangazia maeneo mengine ambayo Tanzania na Ujerumani zinaweza kushirikiana kwa lengo la kuboresha hali ya uhifadhi pamoja na miundombinu katika hifadhi za Taifa.

Aidha, katika ziara hiyo Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.Hamisi Kigwangalla, Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Regine Hess na ujumbe wake walipata fursa ya kutembelea eneo lilipojengwa Kaburi la Askari wa Kingereza aliyeitwa Kepteni Selous ambaye alifariki dunia wakati wa Vita Kuu ya kwanza ya Dunia Januari 4, 1917 na jina la askari huyo kuwa chanzo cha jina la "Selous Game Reserve" - Pori la Akiba la Selous.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post