RAIS MAGUFULI AMTAKA MAKONDA ARUDISHE FEDHA ZA TASAF ALIZOSEMA ALITUMIA KWENDA DODOMA WAKATI SIO MASIKINI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuzirudisha fedha za TASAF ambazo alizitumia vibaya kwa safari ya kwenda Dodoma ili hali sio Masikini.

Rais Magufuli ameyasema hayo hii leo tarehe 17, Febuari, 2020 wakati akizindua kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya mpango wa Maendelo wa kunusuru Kaya masikini wa TASAF. Hafla imefanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dsm.

”Kwenye mpango huu wa TASAF zilijitokeza baadhi ya changamoto, kupitia zoezi la uhakiki wa Kaya Masikini, lililofanyika kuanzia mwezi Novemba 2015 hadi mwezi Juni 2017. Tuliweza kubaini uwepo wa Kaya hewa 73,561.”

”Ambapo Kaya 2234 zilithibitika kuwa wanakaya wake sio Masikini na hapa nafikiri wakina Makonda ambao walizitumia hizi fedha kwenda safari ya Dodoma wakati sio Masikini naomba kama hili ni kweli Makonda azirudishe hizi fedha. Kama ni kweli alitumia fedha za TASAF akaenda nazo huko alipokuwa anaeleza, na yeye hausiki kwenye Kaya Masikini mkae muziangalie hizo fedha lazima azirudishe.”

Kabla ya Rais kutoa kauli hiyo, Makonda alisema mwaka 2012 alipewa nauli na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kwenda mkoani Dodoma kugombea makamu mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM). Amesema fedha hizo zilikuwa sehemu ya mfuko.


“Namshukuru sana mzee Mkapa kuona bado anaendelea kufanya kazi yake, naomba Rais Magufuli niseme mbele yako mfuko huu wa Tasaf nami nimenufaika nao, haikuwa moja kwa moja.”

“Lakini wakati naomba nafasi ya  makamu mwenyekiti wa vijana (UVCCM) Mkapa ndio aliyenipa nauli ya kwenda kuomba kura Dodoma. Kwa hiyo naimani ilikuwa sehemu ya huu mfuko, alikuwa na moyo,” alisema Makonda.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527