MPINA ATOA SIKU 7 VIGOGO SERIKALINI KUKUTANA KUMALIZA DHULUMA KWA WAFUGAJI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akikagua mifugo 600 iliyolundikana kwenye zizi dogo lenye uwezo wa kuhifadhi ng'ombe 60 alipokwenda kukagua mifugo hiyo iliyokamatwa na Halmashauri ya Tanganyika Mkoa wa Katavi na kuwatoza faini ya shilingi milioni 60. Nyuma ni Daktari Mkuu wa Mifugo Tanzania, Profesa Hezron Nonga.
**
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametoa siku saba kwa Daktari Mkuu wa Mifugo Tanzania (CVO), Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Wakili Mkuu wa Serikali wakutane kutathmini na kuondoa dhuluma zinazoendelea kwa wafugaji pamoja na kuandaa kanuni na miongozo itakayoweka uwazi katika usimamizi wa Sheria za Misitu na Mifugo.

Mpina ametoa agizo hilo mwishoni mwa wiki baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi kutoza faini ya shilingi milioni 60 sawa na shilingi laki moja kwa kila ng’ombe baada ya ng’ombe 600 kukamatwa wakichungwa ndani ya  Msitu wa Tongwe Mashariki unaomilikiwa na halmashauri hiyo.

Waziri Mpina amefikia hatua hiyo baada ya kuwepo ukiukwaji mkubwa wa sheria na ukamataji holela wa mifugo unaofanywa kwenye baadhi ya Halmashauri, Hifadhi za Wanyama, Mapori ya Akiba ambapo mifugo inapokamatwa hunyimwa huduma muhimu ikiwemo malisho, maji, chanjo na dawa hali inayosababisha mifugo mingi kudhoofika na kufa.

Alibainisha manyanyaso mengine ni wafugaji kutozwa faini kubwa ambazo hazipo kwa mujibu wa sheria, kupigwa, mifugo kuibiwa, kupigwa risasi na mingine kuuzwa kwa njia ya  mnada kwa kisingizio cha kukosekana mmiliki wa mifugo hiyo huku idadi  inayotajwa mahakamani ni ndogo ikilinganishwa na mifugo iliyokamatwa.

Akizungumza mara baada ya kufika eneo ilikoshikiliwa mifugo hiyo umbali wa zaidi ya kilomita 50  kutoka barabara ya Mpanda- Kigoma, Waziri Mpina alihoji iweje Halmashauri hiyo iache kufuata sheria za nchi zinavyoelekeza kwa watu wanaoingiza mifugo na badala yake wakabuni faini ya kutoka kichwani kinyume cha Sheria na kuitafsiri hatua hiyo kuwa ni Unonevu, Rushwa, Wizi, Dhuluma na Manyanyaso kwa wafugaji.

Waziri Mpina alisema yeye kama msimamizi mkuu wa Sekta ya Mifugo nchini hawezi kumtetea mfugaji anayevunja sheria kwa kuingiza mifugo kwenye maeneo yaliyokatazwa kisheria lakini kilichomfanya kuingilia kati suala hilo ni kuvunjwa kwa Sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002 inayoeleza bayana kwamba mtu atakayekutwa ametenda kosa ndani ya msitu atatozwa faini ya shilingi 30,000 na isiyozidi milioni moja.

“Kutoza hela ambayo haiko kwenye Sheria ni Wizi, ni Manyanyaso kwa wafugaji, Rushwa huwezi kutoza hela ya Serikali ambayo haiko kwenye kanuni yaani Serikali iache kusimamia sheria ifanyie kazi maamuzi ya vikao” alihoji Waziri Mpina.

Mmoja wa wachungaji hao Koye Mmela alilamikia kitendo cha kukamatwa na kushikiliwa msituni kwa siku sita mfululizo bila kufikishwa Mahakamani jambo walilolitaja ni uonevu mkubwa waliofanyiwa na askari waliokuwa doria.

Mwanasheria wa Halmashauri ya Tanganyika, Maraka Mrisho  alimweza Waziri Mpina kuwa faini hiyo ya milioni 60 haipo kwenye sheria yoyote bali ilitozwa kufuatia makubaliano ya kikao kilichowahusisha Maofisa wa Misitu wa halmashauri pamoja na Maofisa wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) wa kanda hiyo na kubariki faini ya shilingi laki moja kwa kila ng’ombe.

Mrisho alisema kwa mujibu wa Sheria ya Misitu Namba Sheria ya Misitu Namba 14 ya Mwaka 2002, kifungu cha 84 Kifungu kidogo cha tano kinasema mtu yeyote atakayekutwa na kosa ndani ya misitu atatakiwa kulipa faini isiyopungua shilingi 30,000 na isiyozidi sh. Milioni 1 hivyo hakuna kifungu kinachozungumia kutoza faini ng’ombe.

Kwa upande wake Daktari Mkuu wa Mifugo Tanzania (CVO),  Profesa Hezron Nonga amesema waliokamata mifugo hiyo wamevunja Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Namba 17 ya mwaka 2003, Sheria ya Ustawi wa Wanyama Namba 19 ya mwaka 2008 kutokana na ng’ombe 600 kulundikana kwenye zizi dogo linalotosha ng’ombe 60 tu hali iliyosababisha mifugo kukosa hewa na kufa, ndama kukanyagwa, kujeruhiwa na kufa.

Prof. Nonga alisema  ng’ombe hao wamefungiwa zizini muda mrefu bila maji wala malisho hali iliyopelekea afya zao kudhoofika, utaratibu wa ukamataji mifugo haukufuatwa kwa kuwa haukuhusisha daktari wa mifugo kama sheria inavyoelekeza huku mifugo hiyo ikinyimwa chanjo na tiba hivyo waliohusika na ukamataji huo walitakiwa kukamatwa na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria hizo.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Rojaz Romuli alisema halmashauri hiyo haina bajeti ya kutibu mifugo pindi inapokamatwa msituni bali jukumu lao ni kulinda misitu isiharibiwe na wavamizi wakiwemo wafugaji na wawindaji haramu.

Hivyo baada ya mazungumzo ya kina ya kisheria na kubainika kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria ndipo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tanganyika, Rojazi Romuli akalazimika kubatilisha adhabu hiyo na kuwatoza faini ya shilingi milioni 11 badala ya shilingi milioni 60 ya hapo awali.

Kwa muda mrefu wafugaji wa Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi wamekuwa wakilalamikia kunyanyaswa, kuteswa kupigwa faini kubwa na hata kuuwawa na kwamba malalamiko hayo yalishatolewa Rais Dk. John Magufuli alipofanya ziara mkoani Katavi mwaka jana.

Pia malalamiko ya aina hiyo yalitolewa kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera waliposhiriki uzinduzi uogeshaji mifugo Halmashauri ya Mpwimbwe mkoani  Katavi.

Homera alilazimika kuchukua hotuba nzima iliyojaa ya malalamiko ya wafugaji na kuikabidhi kwa Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Katavi kwa hatua zaidi lakini bado Halmashauri ya  Tanganyika imeendeleza manyanyaso kwa wafugaji kwa kuwatoza faini kubwa ambazo haziko kwa mujibu wa sheria.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post