Picha : UNDER THE SAME SUN YAZINDUA MRADI WA 'HAKI YETU' KULINDA WATU WENYE UALBINO



Shirika la Under The Same Sun kwa kushirikiana na mashirika wenza GNRC NA CEFA wamezindua mradi wa “HAKI YETU” awamu ya pili, ambao umelenga kupunguza ama kutokomeza kabisa matukio ya kikatili ambayo wamekuwa wakifanyiwa watu wenye ualbino.


Uzinduzi wa mradi huo umefanyika leo Januari 19, 2020 kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga, na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na viongozi wa dini, ambapo mgeni rasmi alikuwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akimwakilisha mkuu wa mkoa Zainab Telack.

Mboneko amesema Serikali inaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha ili mradi huo ufanikiwe kwa asilimia 100, pamoja na kutoa elimu ya kupinga matukio ya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino, kuwaimarishia ulinzi na usalama, kuwapatia hifadhi na elimu katika shule ya Buhangija Jumuishi, pamoja na kufanya msako kwa wale wote wanaotekeleza mauaji na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Amesema bado kuna maeneo mengi katika jamii hayajafikiwa na elimu juu ya uelewa kwa watu wenye ulbino, kwa kutambua hao ni sawa na binadamu wengine, ambacho kinachowatofautisha ni rangi, huku akiahidi Serikali pamoja na wadau watashirikiana kwa pamoja kusambaza elimu hiyo ambayo itapunguza ama kutokomeza matukio ya ukatili na ubaguzi kwa watu wenye ualbino.

“Serikali kwa kushirikiana na wadau itaendelea kutoa elimu ya kupinga ukatili wa mauaji ya watu wenye ualbino, kuimarisha ulinzi na usalama, kuwapa hifadhi, kufanya msako kwa wale wote wanaotekeleza mauaji dhidi yao ama kupanga njama, pamoja na kuwachukulia hatua kali za kisheria,”amesema Mboneko.

“Kutokana na jitihada hizi za kupinga matukio ya ukatili kwa watu wenye ualbino, katika mkoa wetu kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni hakuna tukio lolote lililotolewa taarifa linalohusu mauaji ya watu wenye ualbino, hivyo natoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga wasiwafanye ukatili watu hawa pamoja na kuwabagua,

“Natoa rai pia kwa wazazi na walezi kutowaficha watoto wenye ualbino, bali wawa patie haki zao kama walivyo watoto wengine, ikiwamo kuwapeleka shule, pamoja na kuwapenda,” ameeleza.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya ameziagiza halmashauri zote sita za mkoa wa Shinyanga kuhakikisha zinatenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa mahitaji maalum ya watu wenye ualbino, pamoja na maofisa maendeleo kuwapatia elimu ya ujasiriamali na kuwaunga kwenye vikundi na kuwapa mikopo, ili wapate kufanya shughuli za kuwaingizia kipato.

Naye meneja mradi wa ‘HAKI YETU’ kutoka Shirika la Under The Same Sun Wakyo Musongo, amesema mradi huo unatekelezwa katika mikoa mitano kwa kushirikiana na mashirika matatu ambayo ni Under The Same Sun, GNRC NA CEFA, mikoa ambayo ni Simiyu, Kigoma, Mwanza, Geita pamoja na Shinyanga.

Amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Oktoba mwaka 2019, na sasa wameuzindua katika awamu ya pili mkoani Shinyanga ambapo utakoma Juni mwaka 2021, na utatekelezwa katika halmashauri ya Ushetu pamoja na halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, ambapo watakuwa wakitoa elimu ya kupinga matukio ya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino.

Aidha amesema katika utekelezaji wa mradi huo awamu ya pili kupitia warsha, maonyesho ya sanaa sehemu za wazi, semina, na vyombo mbalimbali vya habari, wanatarajia kufikia watendaji wa serikali 450, viongozi wa dini 400, wanafunzi 30,000, walimu 500, wenye ualbino 250, wananchi 26,000 pamoja na kupitia vyombo vya habari matarajio yao ni kufikia watu 4,000,000.


TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizundua mradi wa 'HAKI YETU' kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack. Mradi huo umelenga kupunguza ama kutokomeza kabisa matukio ya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino. Picha zote na Marco Maduhu - Malunde 1 blog

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi wa 'HAKI YETU' ambao umelenga kupunguza matukio ya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino.

Mkurugenzi wa Shirika la Under The Same Sun Berthasia Ladislaus, akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi wao wa 'HAKI YETU' ambao umelenga kupunguza matukio ya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino, wenye kauli mbiu isemayo Maisha yangu usalama wangu.

Meneja Mradi kutoka Shirika la Under The Same Sun Wakyo Musongo akielezea mradi wa HAKI YETU namna utakavyo fanya kazi mkoani Shinyanga katika kupunguza ama kutokomeza matukio ya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino.

Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt. Rashidi Mfaume akizungumza kwenye uzinduzi huo wa mradi wa HAKI YETU kwa niaba ya katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Albert Msovela. 

Watoto wenye ualbino wakiwa kwenye uzinduzi wa mradi wa HAKI YETU kutoka Shirika la Under The Same Sun.

Watoto wenye ualbino wakiwa kwenye uzinduzi wa mradi wa HAKI YETU kutoka Shirika la Under The Same Sun.

Watoto wenye ualbino wakiwa kwenye uzinduzi wa mradi wa HAKI YETU.

Watoto wenye ualbino wakiwa kwenye uzinduzi wa mradi wa HAKI YETU .

Wadau wakiwa kwenye uzinduzi wa mradi.

Wadau wakiwa kwenye uzinduzi wa mradi.

Wadau wakiwa kwenye uzinduzi wa mradi.

Wadau wakiwa kwenye uzinduzi wa mradi.

Mtoto mwenye ulbino akifuatilia uzinduzi wa mradi kwa kutumia kifaa maalumu cha kuongeza kuona kutokana na kusumbuliwa na tatizo la uoni hafifu.

Wadau wakiwa kwenye uzinduzi wa mradi.

Viongozi wa dini wakiwa kwenye uzinduzi wa mradi.

Mdau wa maendeleo kutoka Shirika la CHIDEP Mathias Chidama akichangia mada kwenye uzinduzi wa mradi wa 'HAKI YETU'.

Mdau wa maendeleo kutoka Shirika la Tawlae Eliasenya Nnko, akichangia mada kwenye uzinduzi wa mradi wa HAKI YETU.

Kikundi cha Dar Creator kikitoa burudani kwenye uzinduzi wa mradi wa HAKI YETU.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko katikati mwenye nguo nyekundu akipiga picha ya pamoja na wafanyakazi kutoka Shirika la Under The Same Sun, pamoja na watoto wenye ualbino.

Picha zote na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527