SERIKALI KUWAWAJIBISHA MAAFISA KILIMO WATAKAOSHINDWA KUSIMAMIA KILIMO

Na Amiri Kilagalila-Njombe
Serikali nchini imesema maafisa kilimo wanatakiwa kumsimamia na kumpa maelekezo mkulima ili kulima kilimo chenye tija,kutokana na wakulima wengi kutumia ardhi kubwa lakini matokeo yanayopatikana yamekuwa hayana tija.


Waziri wa kilimo,ushirika na umwagiliaji Mh.Japhet Hasunga amesema serikali itawawajibisha maafisa kilimo endapo itabainika wakulima wanatumia ardhi kubwa katika kilimo bila ya kutumia maarifa.

Waziri Japhet Hasunga ameyasema hayo wilayani Njombe mkoani Njombe wakati akikagua mradi umwagiliaji wa kikundi cha Twilumba uliopo kijiji cha Itipingi kata ya Igongolo wilayani humo.

“Nataka niwapongeze mliposema mmeongeza tija,mmeniambia mmeongeza kwa mfano nyanya mlikuwa mnapata tani 12 sasa zimefika 30,lakini pamoja na mafanikio hayo nilikopita mashamba yale hayajanivutia kwasababu naona mnavyolima mmeweka hatua kubwa kwa hiyo mnatumia eneo kubwa mavuno kidogo”alisema waziri Hasunga

Kutokana na hilo Waziri hasunga akatumia nafasi hiyo kuwaagiza maafisa kilimo nchini kuwasimamia na kuwaelekeza wakulima ili kubadilisha kilimo.

“Maafisa kilimo hatuko kumshauri mkulima kwa sasa tunatakiwa kumpa maelekezo na kumsimamia,maana sasa hivi nikienda mahali nikakuta wananchi wamelima vibaya hawajatumia maarifa,wanalima kilimo cha hovyo,wanatumia ardhi kubwa tija kidogo wanaotakiwa kuwajibika ni maafisa kilimo kwasababu wao ndio wapo kwenye hayo maeneo”alisema Hasunga

Awali akisoma taarifa ya mradi wa umwagiliaji wa twilumba muweka hazina wa mradi huo Amasinze Kadwame,amesema mradi huo uliojengwa kwa ghalama ya milioni 400 ukiwa na urefu wa mita 1725 una idadi ya wanachama 74 hivyo licha ya upatikanaji wa faida kubwa kutokana na mradi huo wanaiomba serikali kuongeza mradi huo ili kuongeza idadi ya wakulima na mashamba kutokana na uwingi wa maji katika mradi.

“Sisi wakulima kulingana na namna mradi ulivyosanifiwa maji ni mengi tuomba kuongezewa mradi ili kuongeza idadi ya wakulima na mashamba hadi kufika ekari 400 zilizofanikiwa tuongeze uzalishaji na mapato ya halmashauri kupitia ushuru kama serikali inavyohimiza kwa mazao yanayolimwa”alisema Amasinze Kadwame

Nickson Kibiki na Joyce Mbembati ni miongoni mwa wakulima wanaotumia mradi huo,wanasema mradi huo umewawezesha kuongeza uzalishaji ukilinganisha na awali hatua iliyowawezesha wananchi kukuza uchumi wa vipato vyao pamoja na kuwapeleka watoto shule.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527