DKT. NCHIMBI AWAFUNDA TANROADS

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akiwahutubia wataalam wa nchi nzima wa Idara ya Manunuzi wa TANROADS walio katika mafunzo maalum ya mfumo rasmi wa kusimamia mahitaji ya raslimali za matengenezo wa barabara (RMMS) kwenye ukumbi wa VETA mjini Singida leo

Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida Injinia Matari Masige  (aliyesimama) akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi (mwenye skafu) kuwahutubia  wataalam kutoka mikoa yote Tanzania Bara  wa Idara ya Manunuzi wa TANROADS walio katika mafunzo maalum ya  ya mfumo rasmi wa kusimamia  mahitaji  ya raslimali za matengenezo wa barabara (RMMS) kwenye ukumbi wa VETA mjini Singida leo.Kushoto ni Mwezeshaji wa Mafunzo hayo Injinia Mussa George


Picha ya pamoja baina ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi(mwenye skafu) na wataalam wa nchi nzima wa Idara ya Manunuzi wa TANROADS walio katika mafunzo maalum ya mfumo rasmi wa kusimamia mahitaji ya raslimali za matengenezo wa barabara (RMMS) kwenye ukumbi wa VETA mjini Singida leo
 
Na John Mapepele

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amesema ili kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na kukamilisha barabara zote nchini katika kiwango cha lami katika muda mfupi ni muhimu Wakala wa Barabara nchini TANROADS iwashirikishe Wakala wa Barabara vijijini na Mijini (TARURA) kwenye mafunzo maalum ya kuboresha utendaji wa kazi yanayoendelea nchi nzima hivi sasa na kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya hapa kazi tu.

Dkt. Nchimbi ametoa rai hiyo leo kwenye ukumbi wa VETA mjini Singida alipohutubia wataalam wa nchi nzima wa Idara ya Manunuzi wa TANROADS walio katika mafunzo maalum ya ya mfumo rasmi wa kusimamia mahitaji ya raslimali za matengenezo wa barabara (RMMS).

Amesema ameshangazwa kuona katika mafunzo hayo muhimu katika sekta ya uboreshaji miundombinu ya barabara kwa mfumo wa kisasa TARURA hawajashirikishwa wakati mafunzo hayo ni muhimu na yanaongeza tija ya kazi zao.

“Najua nyie mmenolewa vizuri na baba yenu, Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli wakati akihudumu katika Wizara yenu, hivyo hakukuwa na sababu yoyote ya kuwaacha wenzenu katika mafunzo hayo ili kubadirishana uzoefu” alisisitiza Dkt. Nchimbi.

Alisema wataalam wa TANROADS wanauzoefu mkubwa ambao kama watabadirishana na kushirikiana na TARURA wataleta mapinduzi makubwa katika sekta hiyo kwani mfumo huo wa RMMS unatumia raslimali chache na kuleta tija kubwa.

Aidha alisema wakati mwingine kutokana na uzoefu mdogo kumekuwa na changamoto za utengenezaji wa barabara za vijijini kwa wahandisi kuchukua muda mrefu kukamilisha barabara hizo kwa kisingizio cha raslimali fedha ambapo kama wangefundishwa mfumu huu wangeweza kuboresha utendaji wao wa kazi.

Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kuwahutubia wataalam hao, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida, Injinia Matari Masige alisema mafunzo ya mfumo wa RMMS ni nyenzo muhimu kwa tasnia ya ujenzi wa miundo mbinu ya barabara na yanafanyika katika wakati mwafaka.

Alisema kwa mfumo huo wa RMMS hakuna barabara katika nchi ambayo haitafikiwa ambapo pia alisema faida kuu ya mfumo huu unasaidia kutambua mahitaji halisi ya kila barabara hapa nchini.


“Kwa mfumo huu hatutakuwa tena na kitu kama vile hakuna fedha ya ujenzi wa barabara fulani. Sasa tatizo hilo limekwisha” aliongeza Injinia Masige


Mwezeshaji wa mafunzo hayo Injinia Ndaji Mayige alifafanua kwamba kwa mfumo huo kila sehemu korofi zitapata matengenezo kwa wakati na kwamba mfumo huo unarahisisha utoaji wa taarifa za kila eneo.

Alikiri kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa wakala zote mbili na kwamba wataangalia namna bora ya kushirikisha TARURA ili waweze pia kupata mafunzo hayo kwani yatasaidia kuboresha utendaji hadi katika ngazi za vijiji.

Injinia Mayige alisema mafunzo hayo ni ya siku saba ambapo mafunzo kama hayo tayari yameshatolewa kwa kada za Wakuu wa Idara za Mipango na Fedha na Utawala nchi nzima.

Alisema nia ya mafunzo hayo kutolewa nchi nzima ili mikoa yote nchini kuwa na mfumo mmoja utakaorahisisha utendaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527