BENKI YA TPB YAMWAGA VIFAA SHULE ZA SEKONDARI MAMBI NA MAKITA RUVUMA


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Posta Tanzania(TPB) Sabasaba Moshingi wa tatu kushoto akikabidhi moja kati ya meza 100 na viti 100 vyenye thamani ya shilingi Ml 4.8 kwa Mkuu wa wilaya ya Mbinga Cosmas Nshenye kwa ajili ya shule mbili za Sekondari za Mbambi na Makita zilizopo Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma,kushoto Afisa mahusiano wa Benki hiyo Novas Moses. 
BENKI ya Posta Tanzania(TPB) imetoa msaada wa meza 100 na viti 100 vyenye thamani ya shilingi Ml 4.8 kwa shule mbili za Sekondari za Mbambi na Makita zilizopo katika Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma.

Akikabidhi samani hizo za Shule,Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Posta Tanzania Sabasaba Moshingi alisema, Benki hiyo imekuwa na utaratibu wa kutenga kiasi fulani cha fedha kila mwaka na kusaidia jamii hasa katika sekta ya Elimu katika mikoa mbalimbali hapa Nchini.

Alisema, mwaka wa fedha 2019 Benki ya Posta imetenga shilingi milioni 200 kwa ajili ya kuchangia huduma za jamii na itaendelea kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazo fanywa wananchi na Serikali.

Moshingi alisema, Benki ya Posta Tanzania inajivunia sana kuona imekuwa sehemu ya mafanikio katika sekta ya Elimu hapa Nchini na sio mara ya kwanza kuchangia sekta ya elimu kwani mwaka jana ilitumia kiasi cha shilingi milioni 50 kukarabati shule ya Msingi Kindimba iliyopo katika wilaya hiyo.

Amewataka wanafunzi wa shule hizo, kuhakikisha wanatumia meza na viti hivyo kusoma kwa bidi na kujiepusha na mambo yanayoweza kukatisha safari yao ya maisha na kuwataka Watanzania wengine kuunga mkono juhudi zinazo fanywa na Benki ya Posta na Serikali ya awamu ya tano ya kumarisha miundombinu ya Shule.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo Cosmas Nshenye,amewataka wakazi wa Mbinga kuwa wazalendo, na wenye mapenzi mema kwa kumaliza baadhi ya changamoto zinazoikabili wilaya hiyo badala ya kutegemea misaada ya Serikali na wafadhili.

Nshenye ametoa kauli hiyo jana wakati akiongea na wanafunzi,walimu na baadhi ya wananchi katika hafla ya kupokea msaada wa viti 100 na meza 100 zilizotolewa na Benki ya Posta Tanzania kwa shule mbili za Sekondari za Mbambi na Makita wilayani humo.

Alisema, sio jambo la kufurahisha na haipendezi hata kidogo kwa jamii ya wana Mbinga kuona wanashindwa kuchangia ujenzi wa miradi na huduma mbalimbali za kijamii, kwani wana uwezo mkubwa wa kifedha,lakini inasikitisha kuona kazi kubwa ya kuijenga wilaya hiyo imeachwa kwa Serikali na wadau wengine wa maendeleo.

Nshenye alisema, wakati umefika kwa wakazi wa wilaya ya Mbinga kubadilika na kujitolea nguvu kwa kuchangia ujenzi wa miradi ikiwemo miundombinu ya Elimu,Afya,Maji na mingineyo hatua itakayochochea na kuharakisha maendeleo ya Nchi yetu.

Kwa mujibu wake,ni aibu wilaya kama ya Mbinga ambayo wananchi wake wana nguvu kubwa ya kiuchumi inayotokana na zao maarufu la kahawa bado inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa madawati,viti na meza huku baadhi ya wanafunzi wa shule wakilazimika kubeba viti kutoka nyumbani kwao.

Aidha Mkuu wa wilaya ameishukuru Benki ya Posta kwa msaada wa viti na meza ambazo zinakwenda kupunguza mahitaji ya samani kwa shule hizo mbili, ambapo ameyataka makampuni mengine kuiga mfano wa Benki hiyo ambayo imekuwa msaada mkubwa katika kuchangia miundombinu ya shule kwa wilaya ya Mbinga.

Amewataka wanafunzi kutumia meza na viti hivyo kusoma kwa bidii, hali itakayowasaidia kufikia malengo waliyojiwekea katika safari yao ya maisha nan a viti na meza hizo wazitumie kama chachu ya mafanikio.

Awali Mkuu wa shule ya Makita Wilson Msengi alisema, shule hiyo ina upungufu wa viti 62 na meza 58,lakini msaada huo uliotolewa na Benki ya Posta utapunguza sana changamoto hiyo.

Alisema,samani hizo zinakwenda kuhamasisha suala zima la kujifunzia na kufundishia darasani na pia kuchochea taaluma kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527