WAZAZI WALIA NA WAMILIKI WA SHULE SINGIDA, WATOTO WAO KUCHELEWA KUREJEA NYUMBANI


Na Abby Nkungu, Singida.
WAZAZI wa watoto wanaosoma shule za awali za mchepuo wa Kiingereza katika Manispaa ya Singida, maarufu "English Medium" wameiomba Serikali kuwalazimisha wamiliki wa shule za Maasai,Abeti, Maemack na Malaika wa Matumaini kuwa na magari ya kutosha kwa ajili ya kuwapeleka shuleni na kuwarejesha majumbani watoto wao kwa muda muafaka.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wazazi wamesema kuwa watoto wao wanaosoma kutwa katika shule hizo hulazimika kuamka majira ya saa 11:00 alfajiri kila siku za masomo kwa ajili ya kujiandaa kwenda shule na huchelewa kurejea majumbani hadi saa 11 jioni.

"Hebu fikiria, kwa mtoto wa shule ya awali mwenye umri wa chini ya miaka sita kulazimika kuamka kila siku saa 11 alfajiri na kurejea nyumbani saa 11 jioni, kesho yake vivyo hivyo; hakika mtoto anachoka na kumfanya achukie shule kwa kuona kama vile anapewa adhabu” alisema Sakilu Ntandu, mmoja wa wazazi.

Sakilu anaeleza kuwa, moja ya sababu kubwa inayochangia watoto wao kuamka mapema ni uhaba wa mabasi ya shule hizo, hivyo gari moja hulazimika kuanza mzunguko wa kukusanya watoto mapema kuwapeleka shule ili kurudi kuchukua wengine. Vivyo hivyo, wakati wa kuwarejesha nyumbani jioni.

“Kuna wakati mtoto anachoka kupitiliza, unamwamsha hiyo saa 11 alfajiri, unamnawisha, unamvisha nguo na kumpakia kwenye gari ukidhani yuko macho kumbe bado anachapa usingizi” alisema mzazi huyo na kuongeza kuwa kuna baadhi ya shule hizo hazina hata sehemu ya watoto kupumzika baada ya kupata chakula cha mchana hivyo mtoto huendelea kuteseka mchana kutwa.

Mzazi mwingine, Kidoho Kidimanda alieleza kuwa licha ya kumuamsha mtoto wake alfajiri, wakati mwingine dereva wa shule haendi kumpitia kwenye Kituo kilichokubaliwa hali inayomlazimu aingie gharama nyingine ya kumpeleka shule yeye mwenyewe au huamua kurudi naye nyumbani; hivyo kumkosesha masomo siku hiyo.



Kutokana na hali hiyo, wazazi hao wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwalazimisha wamiliki wa shule hizo kuwa na idadi ya magari kulingana na wingi wa wanafunzi ili kukidhi mahitaji ya kuwapeleka shule na kuwarejesha nyumbani kwa wakati ikiwa ni njia mojawapo ya kuboresha mazingira ya mtoto kupenda kwenda shule na kujifunza katika hatua za awali.





Uchunguzi zaidi wa Mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa uhaba wa magari katika shule hizo umezaa tatizo lingine la wanafunzi kujazana kupita kiasi kwenye gari moja.



Changamoto hiyo ni watoto kujazana kupindukia hadi wengine hukaliana mapajani hali ambayo ni hatari kiafya na ni kinyume na Sheria za Usalama barabarani; isitoshe, hawajifungi mikanda kutokana na magari hayo kukosa viti maalum kwa ajili ya watoto, jambo ambalo ni hatari iwapo ajali itatokea.





Akiongea kwa niaba ya Ofisa Elimu Taaluma shule za Msingi Manispaa ya Singida, Ofisa elimu Vielelezo Fatina Kipingu alikiri kuwa na taarifa juu ya baadhi ya shule hizo ambazo wanafunzi wake husoma kutwa hazina mabasi ya kutosha hivyo wameanza kulifanyia kazi suala hilo.





Wataalam wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto wanasema mtoto anapaswa kupumzika angalau kwa saa moja hadi mbili awapo shuleni na kwa shule zinazokaa na watoto kwa saa nyingi lazima ziwe na ratiba yenye huduma ya mapumziko; ikiwemo kulala kwa muda kwa kuwa kupumzika ni afya kwa mtoto kwani ubongo wake bado unakua kwa kasi. MWISHO








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527