RAIS MAGUFULI KUANZA ZIARA DODOMA KESHO


ZIARA YA KIKAZI YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MKOANI DODOMA

Ndg. Waandishi wa Habari
Natumia fursa hii kuwatangazia wananchi wote wa Mkoa wa Dodoma na umma wa Tanzania kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, imempendeza kufanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Dodoma, Makao Makuu ya nchi, kuanzia tarehe 21 hadi 25 Novemba, 2019.

Katika ziara yake Mkoani Dodoma, Mhe. Rais atatembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwenye Mkoa wa Dodoma. Vilevile, atatumia ziara yake kuzungumza na wananchi wa Mkoa wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla kupitia Mikutano kadhaa ya hadhara ambayo  hotuba hizo zitarushwa moja kwa moja (mubashara) kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Ndg. Waandishi wa Habari

Miongoni mwa shughuli atakazofanya ni kama ifuatavyo:-

Alhamisi Novemba 21, 2019, Mhe. Rais atakuwa ni Mgeni Rasmi katika Mahafali ya kumi (10) ya Chuo Kikuu cha Dodoma – UDOM yatakayofanyika kwenye ukumbi wa Chimwaga, Chuoni hapo.

Ijumaa Novemba 22, 2019 Mhe. Rais atatembelea na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya Hospitali ya Uhuru, Wilayani Chamwino; ujenzi wa nyumba 118 za Askari Polisi katika maeneo ya FFU Nzuguni na Medeli East; Ujenzi wa Stendi Kuu ya mabasi iliyopo Nzuguni; na Soko Kuu linalojengwa katika eneo la Nzuguni na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika katika stendi ya mabasi Nzuguni. 

Jumatatu Novemba 25, 2019 Mhe. Rais ataweka mawe ya msingi kwenye miradi ya ujenzi wa Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi Tanzania Kikombo; ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji na Ujenzi wa jengo la Makandarasi katika eneo la National Capital City.

Ndg. Waandishi wa Habari

Maandalizi yote yamekamilika na Sisi wana Dodoma, kama ilivyo kwa watanzania wote, tunaelewa fika wingi na uzito wa majukumu aliyonayo Mhe. Rais ya kujenga Tanzania mpya na yenye matumaini makubwa kimaendeleo na ustawi wa Jamii. Hivyo, kupata nafasi ya kufanya ziara kwenye Mkoa wa Dodoma, licha ya majukumu hayo, ni upendeleo usiokuwa na kifani. Hivyo kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma, nitumie fursa hii kumshukuru sana Mhe. Rais kwa upendeleo anaotupatia daima.

Ziara hii ya Mhe. Rais kwetu ni fursa ya kumwonesha hatua tulizofikia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo aliyotupatia na kupokea maelekezo ya namna ya kusonga mbele kwa uhakika katika hatua mbalimbali za utekelezaji wake. Aidha, atatumia ujio huu kuelekeza yale atakayoona kuwa yatazidi kuboresha utendaji wetu na yatakayotupa shime na hamasa zaidi ya kusonga mbele zaidi kimaendeleo. Hivyo, wananchi wa Dodoma tujitokeze kwa wingi kuungana na Rais wetu mpendwa na hivyo, kufanikisha ziara yake.

AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA!

Dkt. Binilith S. Mahenge
MKUU WA MKOA
NOVEMBA 20, 2019


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post