BENKI YA MAENDELEO YA AFRIKA KUSAIDIA UJENZI WA MIRADI YA NISHATI TANZANIA

Na Benny Mwaipaja, Johannesburg

BENKI ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeahidi kuendelea kuisadia Tanzania kutekeleza miradi yake mikubwa ya kimkakati hususan miundombinu ya Nishati na Barabara kwa kuendelea kuipatia mikopo yenye masharti nafuu ili kuharakisha maendeleo ya nchi.

Ahadi hiyo imetolewa Mjini Johannesburg nchini Afrika ya Kusini na Kaimu Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayesimamia Miundombinu ya nishati, Bw. Wale Shonibare alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, kando ya Kongamano la Pili la Jukwaa la Uwekezaji Afrika lililoandaliwa na Benki hiyo.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mkutano wao, Dkt. Mpango amesema kuwa ameiomba Benki hiyo kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kipaumbele inayojengwa na Serikali hususan katika Sekta za nishati, barabara, uongezaji thamani wa mazao ya kilimo, elimu na maji.

Dkt. Mpango ameitaja miradi iliyowasilishwa kwa kiongozi huyo kuwa ni mradi wa kuzalisha umeme wa Ruhudji (MW 358), mradi wa umeme wa Rumakali (MW 222) mradi wa umeme wa mto Malagarasi (MW 44.5), Mradi wa kuzalisha umeme wa Kakono (MW 87) na miradi mingine ambayo itajadiliwa na Bodi ya Benki hiyo itakayokutana mwishoni mwaka huu.

Amesema kuwa miradi hiyo mikubwa itakayoiwezesha nchi kuwa na umeme wa kutosha ni muhimu kwani itasaidia kufanikisha agenda ya Seikali ya kuwa na uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

“Tumewakaribisha waje Tanzania kwa ajili ya mazungumzo na kujionea namna miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo vingine kama umeme jua na ule unaozalishwa kwa njia ya upepo kama ilivyo katika maeneo mengine ya Afrika hususan Kusini mwa Jangwa la Sahara” alisisitiza Dkt. Mpango

Amesema kuimarika kwa Sekta ya nishati nchini kutaleta manufaa makubwa ikiwemo kuziwezesha biadhaa za kilimo kama vile pamba kuongezewa thamani kutokana na kuwepo kwa umeme wa uhakika wa kuendesha viwanda.

Kwa upande wake Kaimu Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Bw. Wale Shonibare, amesema kuwa Benki yake iko tayari kuisaidia Tanzania ili ifikie mapinduzi makubwa ya miundombinu ya nishati kutokana na umuhimu wake katika kuendesha uchumi.

Alisema nishati ni jambo muhimu ili nchi iweze kufikia mapinduzi ya viwanda na aliahidi kufanya kila linalowezekana kuhakikisha Benki yake inachangia juhudi za serikali za kuongeza uwezo wa kuzalisha umeme, kujenga njia za kusafirishia umeme na usambazaji wake kwa kulijengea uwezo Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO)

Mwisho


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post