AGIZO LA RAIS MAGUFULI LATEKELEZWA NDANI YA SAA 24.....TAASISI 4 ZATOA GAWIO LA BILIONI 2.75


Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Saa chache baada ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kutoa siku 60 kwa Taasisi, Kampuni ambazo Serikali ina hisa chache na Mashirika ya Umma 187 ambayo hayajatoa gawio au mchango kwa Serikali tayari Taasisi nne zimetekeleza agizo hilo leo.


Akizungumza leo, jijini Dodoma, wakati akipokea gawio na michango kutoka Shirika la Posta, Shirika la Reli (TRC), Self Microfinance Fund, na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), ambapo jumla ya fedha zilizowasilishwa ni shilingi bilioni 2.75, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango alisema kuwa baada ya agizo la Rais alilolitoa jana, hakutakuwa na mzaha kwa Taasisi, Kampuni na Mashirika ambayo hayatekeleza agizo hilo ndani ya siku 59 zilizobaki.

“Nitasimamia kikamilifu agizo hili la Mheshimiwa Rais, itakapofika siku ya 60 nitatembeza panga bila uoga wala kupepesa macho kwa Taasisi, Kampuni na Mashirika ambayo hayatakuwa yametekeleza agizo hili, hatutanii katika hili” alisema Waziri Mipango.

Aidha, Waziri Mpango alizishukuru Taasisi hizo kwa kutekeleza agizo la Rais na kuongeza kuwa angependa kuona Mashirika yaliyobaki yakitekeleza agizo hilo kwa wakati, kwa kuwa fedha hizi si zake wala za Rais bali ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa faida ya watanzania wote.

Naye, Msajili wa Hazina, Athumani Mbutuka alisema kuwa alitekeleza agizo la Rais Magufuli la kumtaka kuzijulisha Taasisi, Kampuni na Mashirika 187 ambayo hayakuwa yametoa gawio na michango kufanya hivyo ndani ya siku 60, ambapo Taasisi za TRC, TIC, Shirika la Posta na Self Microfinance Fund  wamekuwa wa kwanza kutekeleza agizo hilo.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli jana alipokea gawio na michango kutoka kwa Taasisi, Kampuni na Mashirika 79 ambayo yalitoa jumla ya shilingi trilioni 1.05, ambapo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro, Wakala wa Huduma za Misitu na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) yalikabidhiwa cheti kwa kufanya vizuri. Aidha, TPA iliyotoa gawio la shilingi bilioni 169 na TPC iliyotoa shilingi bilioni 14 yalipewa tuzo kwa  kutoa gawio kubwa zaidi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527