SERIKALI YASHTUKIA KUSUASUA KWA UENDESHAJI KIWANDA CHA TANGA FRESH

Na. Edward Kondela

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeshtukia kusuasua kwa uendeshaji wa kiwanda cha Tanga Fresh hali iliyolazimu kuundwa tume kufanya uchunguzi wa namna kiwanda kinavyofanya kazi ikiwemo kuchunguza mtambo unaotumika kusindika maziwa ya muda mrefu ambao unadaiwa umekuwa ukiongeza gharama ya uendeshaji wa kiwanda hicho.

Akizungumza jana (21.10.2019) katika kiwanda cha Tanga Fresh mjini Tanga, kwenye kikao kilichohusisha menejimenti ya kiwanda pamoja na wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU) kinachomiliki asilimia 43 ya kiwanda hicho.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amefafanua kuwa serikali itahakikisha inachukua hatua kunusuru kiwanda kufuatia ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli alipotembelea kiwanda hicho mwaka 2017 na kuahidiwa na menejimenti kusindika maziwa lita laki moja kwa siku ambapo katika ziara hiyo Rais Magufuli aliwasaidia kupata hati iliyokuwa imekwama kwa miaka mingi, kuondoa changamoto ya wanahisa juu ya hisa zao Tume ya Ushindani (FCC) hali iliyopelekea kiwanda  kuanza kujitanua na kuongeza uzalishaji wa maziwa ya muda mrefu (UHT) ingawa kiwanda kiliamua kuchukua mkopo Benki ya Biashara (NMB), unaoonekana kuwalemea na kutofanya vizuri sawa na ahadi kwa Rais Magufuli.

“Kwanza serikali imebaini manunuzi ya mtambo wa kusindika maziwa ya muda mrefu kuwa ni mtambo uliyokwishatumika na umenunuliwa kwa zaidi ya Shilingi Bilioni Sita, pia riba ya mkopo kuwa ni kubwa na kuwa mzigo, hivyo nimeagiza iundwe tume ambayo tayari Mkuu wa Mkoa wa Tanga ameiunda kuanzia leo kufanya uchunguzi wa mtambo ulionunuliwa ikiwemo fedha ya kununulia mtambo huo na utaratibu uliotumika kununulia mtambo.” Amesema Mhe. Ulega

Aidha Mhe. Ulega ameitaka bodi ya wakurugenzi wa kiwanda pamoja na wamiliki wakae pamoja na Benki ya Kilimo (TADB) kuitaka benki hiyo kununua deni hilo ili kutoa nafuu kwa kiwanda na kuondoa mzigo kwa wafugaji na kuinua kipato chao.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bw. Martine Shigella amesema tayari timu ya wataalamu wakiwemo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Viwanda na Maendeleo (TIRDO) imeshaundwa ili kubaini hali ya mtambo wa kusindika maziwa. 

Bw. Shigella amefafanua kuwa serikali itachukua hatua kwa yeyote atakayebainika kukihujumu Kiwanda cha Tanga Fresh ikiwemo kununua mtambo wa kusindika maziwa usio na tija kwa kiwanda hicho.

Nao baadhi ya wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU) wamepongeza hatua zilizochukuliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na uongozi wa Mkoa wa Tanga kutafuta suluhu ya namna ya kuboresha Kiwanda cha Tanga Fresh ili kiweze kuongeza uzalishaji na kuwanufaisha wafugaji ambao wamekuwa wakiuza maziwa katika kiwanda hicho pamoja na kutaka kiwanda hicho kiongeze bei ya kununua maziwa kutoka kwa wafugaji hao ambao hawaridhiki na bei ya Shilingi 700 kwa lita moja.

Kikao baina ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, uongozi wa mkoa wa Tanga, menejimenti ya kiwanda cha Tanga Fresh, bodi na wamiliki wa kiwanda kinatarajiwa kuendelea hii leo (22.10.2019) ili kutafuta suluhu ya kunusuru kiwanda hicho baada ya kupata hasara kwa miaka mitatu mfululizo.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527