RAIS MAGUFULI AAAHIDI KUENDELEA KUMUENZI MWALIMU NYERERE



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia kwenye sherehe za Kilele za Mbio za Mwenge, Wiki ya Vijana na Kumbukizi ya Miaka 20 ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere katika Uwanja wa Michezo wa Ilulu Mjini Lindi Oktoba 14, 2019
**
Rais  Magufuli ameahidi kuwa serikali ya awamu ya tano itaendelea kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere bila uoga wowote kwa kutekeleza mambo mbalimbali ambayo alitamani kuyafanya enzi za uhai wake.


Ametoa ahadi hiyo leo Jumatatu Oktoba 14, alipokuwa akihutubia wananchi katika hafla ya maadhimisho ya kilele cha mbio za mwenge wa uhuru, kumbukizi ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na wiki ya vijana kitaifa inayofanyika katika uwanja wa Ilulu Mkoani Lindi.

“Serikali ninayoingoza itaendelea kumuenzi Baba wa Taifa, kuheshimu tunu za mwenge pamoja kuendelea kuwathamini vijana ikiwemo kuwateua kushika nafasi mbalimbali za uongozi na wito wangu kwa vijana watakaoteuliwa kushika nafasi hizo wajitahidi kufanya kazi kwa bidii na uzalendo mkubwa,”.

“Tumejitajidi kumenzi Baba wa Taifa kwa kupambana na vitendo vya rushwa, wizi, ubadhilifu wa mali za umma mambo ambayo aliyachukua enzi za uhai wake na katika hilo tumeanzisha kitengo maalumu cha mahakama cha kushugulikia mafisadi pia tumeondoa watumishi hewa takribani 20,000 na wafanyakazi wenye vyeti vya kughushi takribani 14,000,”

“Ili kuendelea kuenzi mchango mkubwa uliotolewa na Baba wa Taifa hatuna budi kuwafundisha vijana wetu kuhusu mambo muhimu ambayo yalisimamiwa na baba wa Taifa katika uhai wake ikiwemo uzalendo, uaminifu, nidhamu, uchapakazi na moyo wa kujitolea kwani tusipofanya hivyo tutakuwa tumeliangamiza taifa letu kwasababu vijana ni kundi kubwa na ndio viongozi wa leo na kesho,” amesema Rais Magufuli.

Aidha amewataka Watanzania kumuishi Mwalimu Nyerere kwa kutimiza maono yake aliyotamani kuyatimiza, kusimamia miiko ya azimio la Arusha pamoja na kudumisha umoja bila kubaguana kwa dini waka kabila.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527