WANAWAKE WAPEWA MBINU ZA KUSHINDA UCHAGUZI


Mwezeshaji wa Mafunzo Bw. Henry Kigodi akifafanua jambo katika mafunzo 
Mwezeshaji Gratiana Rwakibarila akiwa anaeleza namna ya kuboresha mbinu za kampeni 
Washiriki wa mafunzo wakiwa katika vikundi vya mijadala 
WANAWAKE wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma waliotia nia ya kugombea uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika nchini Tanzania, Novemba 24, 2019 toka vyama vya siasa wamepewa mbinu za kushinda uchaguzi huo kwa wingi na kishindo.

Wanawake 64 wamepewa mafunzo na Shirika lisilo la Kiserikali la Tanzania Gender Networking Programme (TGNP Mtandao) la Dar es Salaam, kwa lengo la kuwajengea uwezo wanawake waliotia nia katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi wa serikali za mitaa wakiwa na moto wao wa "Wanawake wakati wa kuongoza ni sasa".
Mwezeshaji wa Mafunzo hayo toka TGNP Mtandao, ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere Dar es Salaam, Bw. Henry Kigodi amesema: TGNP Mtandao imejikita kusaidia wanawake ambao wametia nia katika kugombea nafasi mbalimbali ili kukidhi hitaji la kupata viongozi wanawake wengi ambao kwa kipindi kirefu hushindwa kufanikiwa kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukosa mbinu za kampeni na kukabiliana na mfumo dume. 

Bw. Kigodi alisema wanawake wakipata uongozi huwa makini katika maamuzi, kutekeleza na kusimamia shughuli za kimaendeleo kwakuwa wanawake huwa wanakabiliwa na changamoto nyingi za kimaendeleo katika vitongoji, vijijiji na mitaa yao. “Wanawake ndiyo wanaohangaika na changamoto za ukosefu wa maji, huduma za afya na Malezi lakini wao ndiyo hushiriki kwa kiwango kikubwa katika shughuli za uzalishaji mali kama kilimo na hawafaidi matunda yake,” alisema Kigodi.

Naye, mwezeshaji Mwenza Gratiana Rwakibarila, alisema ni vema wanawake wakatambua kuwa wana uwezo mkubwa katika kuongoza jamii na hivyo wanawajibu mkubwa katika kuhakikisha wanapata mbinu za kushinda nafasi walizoziomba kwa kupewa mafunzo ya kujijengea uelewa wa pamoja juu ya ushiriki katika uchaguzi.

Vilevile alisema, wanawake lazima wajengewe uelewa wa dhana za jinsia ili kuwawezesha watia nia kuzihusisha na masuala ya uchaguzi, kujadili umuhimu katika ushiriki wa wanawake katika kampeni na uchaguzi. Aidha, Gratiana alisema mafunzo hayo yatawaboreshea mbinu zao za mikakati na mbinu za kampeni wakati wa uchaguzi.

Jumla ya vyama vitano vya siasa vinashiriki mafunzo hayo, vyama hivyo ni ADA- TADEA, CCM, CHADEMA, CUF na TLP. 

Washiriki wamesisitizwa kuwa wakishinda wayaangalie maendeleo kwa mtazamo wa kijinsia na kupambana na sera potofu za kijinsia.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo (MB), maandalizi ya awali ya uchaguzi wa serikali za mitaa yamekamilika kwa kuzingatia kanuni za Uchaguzi wa serikali za Mitaa wa Mwaka 2019 Ibara ya 4 (13).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527