WAZIRI MKUU: WALIOZEMBEA AJALI YA MOTO MOROGORO WACHUKULIWE HATUA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezielekeza mamlaka husika ziwachukulie hatua za kinidhamu watu wote ambao hawakutekeleza majukumu yao ipasavyo kufuatia tukio la ajali ya moto iliyotokea Agosti 11, 2019 mkoani Morogoro na kusababisha vifo vya watu 104, majeruhi pamoja na uharibifu wa mali.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Septemba 13, 2019) , wakati akiahirisha mkutano wa 16 wa Bunge la 11, Bungeni jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi tarehe 3, Novemba mwaka huu.

“Baada ya tukio hilo la kusikitisha tarehe 12 Agosti 2019niliunda Kamati Maalumu kwa lengo la kufanya uchunguzi wa kina kuhusu ajali hiyo iliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.”

“Lengo lilikuwa kufahamu chanzo cha ajali, mazingira baada ya ajali na hatua gani zichukuliwe kuzuia matukio kama haya sambamba na kuwawajibisha wale wote ambao hawakutekeleza wajibu wao ipasavyo kabla na baada ya ajali kutokea.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwashukurumadaktari na wahudumu wa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili nawadau wote ambao walishiriki kuokoa maisha ya waathirika wa ajali hiyo tangu ilipotokea.

“Nawasihi Watanzania wenzangu tujifunze kutokana na ajali hiyo iliyotokea Morogoro na hivyo kuepuka mikusanyiko ya aina hiyo katika maeneo ya ajali. Aidha, tujenge nyoyo za huruma na kuwa wepesi wa kutoa msaada kwa waathirika wa ajali badala ya kutumia kama fursa za kujinufaisha isivyo halali.”

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527