WAZIRI LUGOLA AWATAKA WANANCHI KUTOA TAARIFA ZA WAHAMIAJI HARAMU KUONDOA UJAMBAZI, UTEKAJI MIKOA YA MIPAKANI NCHINI


Na Felix Mwagara, MOHA-Katavi
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewataka wananchi wa mikoa ya mipakani nchini kutoa taarifa za wahamiaji haramu ili kudhibiti matukio ya ujambazi, utekaji katika maeneo hayo.


Lugola alisema uhalifu katika mikoa hiyo licha ya kuwa imethibitiwa kwa kiasi kikubwa lakini bado baadhi ya mikoa ukiwemo Mkoa wa Katavi, wahalifu utumia njia zisizo rasmi kuingia nchini na kufanya matukio ya uhalifu.

Akizungumza na mamia ya wananchi wa Kijiji cha Ikola, Wilayani Tanganyika, Mkoa wa Katavi, leo, Lugola aliwataka wananchi hao kutoa taarifa kwa vyombo vya dola, kwa mtu au watu ambao wanawatilia mashaka ili kudhibiti matukio mbalimbali ya uhalifu.

“Mnapaswa kuwa wazalendo kwa kutoa taarifa za wahamiaji haramu katika maeneo yenu ili kuisaidia serikali yenu kuwasambaratisha wahamiaji haramu ambao wanafanya uhalifu wakishirikiana na Watanzania wasiowaaminifu waishio mipakani, hii haiwezekani, na kamwe Serikali haiwezi kuchezewa,” alisema Lugola.

Lugola aliongeza kuwa, Tanzania ina Serikali ambayo ipo makini katika kuwalinda watu wake, hivyo kwa majambazi ambao wanafanya matukio mbalimbali ya utekaji lazima washughulikiwe ipasavyo bila kuonewa huruma.

“Wahamiaji haramu wapo mitaani kwetu, na mnawajua, hivyo mnapaswa kutoa taarifa kwa maafisa uhamiaji, Jeshi la Polisi au vyombo vingine vya dola nchini, ili Serikali ya Dkt. Magufuli iweze kuwatia mbaroni haraka iwezekanavyo,” alisema Lugola.

Kwa upande wake, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Katavi, Kamishna Msaidizi, Vicent Haule alikiri kuwepo na changamoto hiyo, na kuahidi kuwasaka wahamiaji haramu kupitia vyanzo vyote vya uchunguzi.

Haule alisema maeneo ya mipakani yana changamoto licha ya kuwa ofisi yake inafanya kazi usiku na mchana kupambana na wahamiaji haramu, na wapo tayari kupokea taarifa za wahamiaji hao watakapopewa na wananchi.

“Tunamshukuru sana mheshimiwa Waziri kwa kutupa maelekezo mbalimbali, hasa ya kuhusu masuala ya wahamiaji haramu, na uraia hasa pale makazi ya Katumba na Mishamo, kwasababu amewataka wakazi waliopewa uraia wasivunje sheria za nchi kwa kwenda Burundi na kurudi nchini bila kufuata sheria,” alisema Haule.

Aidha, Lugola aliwataka Polisi kuwasaka na kuwakamata majambazi na kuwasambaratisha bila woga wowote maana mhalifu hawezi kuchekewa.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Lilian Matinga, alimshukuru Waziri Lugola kwa kufika katika wilaya hiyo na kuahidi maagizo yote aliyoyatoa kwa Wilaya hiyo watayafanyia kazi kupitia vikao vyao vya kamati ya ulinzi na usalama.

Waziri Lugola amemaliza ziara yake Mkoani Katavi kwa ksuikiliza kero mbalimbali za wananchi kupitia mikutano ya hadhara na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527