Waziri Kairuki Aipa Siku Saba TIC Kuwafikia Wawekezaji Wazawa



NA MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika masuala ya Uwekezaji nchini Mhe.Angellah Kairuki ameutaka uongozi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kutembelea na kugakua mazingira ya wafanyabiashara na wawekezaji wazawa waliopo mkoa wa Ruvuma ndani ya siku saba.

Ametoa kauli hiyo alipotembelea na kukagua kiwanda cha kutengeneza kahawa cha Wilaya ya Mbinga cha MCCCO pamoja na kiwanda cha DAE kwa lengo la kukagua mazingira na utendaji wa viwanda hivyo Mkoani Ruvuma.

Ziara hiyo iliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe.Christina Mdeme pamoja na watendaji kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Viwanda, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Nishati, Wizara ya Madini, Wizara ya Ardhi, pamoja na baadhi ya taasisi za serikali ikiwemo na Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC).

Waziri Kairuki alitoa maelekezo hayo baada ya kubaini kuwa kituo hicho  hakijawafikia wawekezaji wazawa kikamilifu hususani waliopo mikoani ili kuwatambua na kuwaelimisha kuhusu fursa zinazotolewa na taasisi hiyo.

 “Ninawaagiza TIC mfike katika viwanda hivi ndani ya siku saba kuanzia sasa ili kuwatembelea na kuwaeeleza huduma zinazotolewa na taasisi yenu ikiwemo fursa zilizopo na endapo wataona inafaa wajisajiri kwa kuwa ni suala la  hiari,”alisisitiza Waziri Kairuki

Aidha alieleza kuwa ipo tija ya kuwatambua wawekezaji wazawa waliopo nchini ka kuzingatia mchango wao katika uchumi wa viwanda kwa kuzingatia mwaka 2019 ni mwaka wa uwekezaji.

“Naelewa kuwa ipo miradi mingi iliyofikiwa na TIC zaidi ya asilimia 72 hivyo niwatake mfike haraka mkoani Ruvuma hususan katika viwanda hivi vya kahawa, ili kuvitambua na kueleza fursa na umuhimu wa kujisajili na Taasisi hii ili kuendelea kuchangia na kuwa na tija zaidi katika uchumi wa nchi,”alisisitiza

Mkurugenzi wa Sera Mipango na Utafiti wa TIC Mafutah Bunini amesema katika kuboresha utendaji wao wamefungua ofisi za kanda saba ili kuwafikia kwa urahisi wawekezaji wa ndani na kwamba wanaotoa uzito sawa kwa wawekezaji wa ndani na nje.

“Na katika hili ndiyo maana viwango vya mitaji ya uwekezaji vinatofautiana kwa wawekezaji wa nje na ndani ambapo mwekezaji wa ndani anatakiwa awe na mtaji wa dola laki moja lakini mwekezaji wa nje ni dola laki tano.

Naye Meneja wa Kiwanda cha kutengeneza kahawa cha Wilaya ya Mbinga (MCCCO) amemuahakikishia Waziri kuwa wataendelea kuboresha mazingira mazuri ya wafanyakazi na kuongeza thamani ya bidhaa zao za kahawa na kuhakikisha jamii iliyowazunguka inanufaika na kiwanda hicho.

“tunaishukuru Wizara ya Uwekezaji kwa jitihada inazofanya za kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuondoa vikwazo mbalimbali vilivyokuwepo awali hali inayosababisha uwekezaji kukua kwa kasi”

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha kutengeneza kahawa cha DAE Bw. Danistan Komba ambaye pia ni mkulima wa kahawa alimpongeza waziri kwa kutembelea kiwandani hapo na kueleza changamoto za masoko ya kahawa na kuiomba Serikali kuendelea kuwaangalia wawekezaji hao wazawa.

“Kipekee napongeza ujio wako, japo tunachangamoto ya masoko kwa kuzingatia kiwanda kina uwezo wa kuzalisha tani 36,000 kwa mwaka na kuuza katika baadhi ya nchi,”alieleza Komba

Alifafanua kuwa, pamoja na changamoto za uhaba wa masoko, kiwanda kimekuwa kikishiriki katika maonesho ya nchi zinazolima kahawa ikiwemo Kenya, Uganda,Rwanda,Burundi na Ethiopia.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Cosmas Nshenye alieleza kuwa, ziara hiyo imeleta chachu kwa wafanyabiashara na wawekezaji wazawa kwa kuzingatia kuwa, Serikali imeahidi kutoa ushirikiano wa kina katika kutatua changamoto zao ikiwemo kuwataka TIC kufika na kuwatembela katika muda alioagiza.

=MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments