WAFANYA BIASHARA 10 KUTOKA RWANDA WATINGA KUWEKEZA MKOANI KAGERA

Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia jenerali Elisha Marco Gaguti akiwa katika picha ya pamoja na wafanya biashara kutoka Rwanda 

Na Lydia Lugakila - Malunde 1 blog

Kundi la Wawekezaji 10 ambao ni Wamiliki wa makampuni mbalimbali ya biashara nchini Rwanda walioamua kuunda Kampuni moja ya uwekezaji wamewasili mkoani Kagera ili kuchangamkia fursa ya uwekezaji mkoani Kagera katika Sekta ya ufugaji wa kisasa na kuanzisha kiwanda cha kusindika nyama.

Wawekezaji hao wamewasili mkoani Kagera leo Septemba 11,2019 na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti ili kumweleza nia yao na kuwa wapo tayari kuwekeza katika ufugaji na kiwanda cha kusindika nyama.

Ujio wa wawekezaji hao ni sehemu ya Jitihada za viongozi wa mkoa wa Kagera kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha uchumi wa nchi za Afrika Mashariki ikiwa ni mafanikio yaliyopatikana kutokana na Wiki ya Uwekezaji Kagera kumalizika hivi karibuni iliyolenga kuonesha fursa mbalimbali za uwekezaji mkoani humo.

Kiongozi wa wawekezaji hao kumi kutoka nchini Rwanda,William Kawamala amemweleza Mkuu wa Mkoa Gaguti kuwa wapo tayari kuwekeza katika sekta ya ufugaji wa kisasa wa ng’ombe katika Kampuni za Ranchi za Taifa (NARCO) baada ya kupata fursa hiyo katika Wiki ya Uwekezaji Kagera iliyofanyika tarehe 12 hadi 17 Agosti, 2019.

“Sisi baada ya kushiriki Wiki ya Uwekezaji Kagera tulivutiwa kuwekeza katika Sekta ya ufugaji, na tuliporudi kwetu nchini Rwanda tulikaa pamoja na kukubaliana tujiunge kwa pamoja wafanyabiashara kumi ili kuanza uwekezaji mara moja, ndiyo maana tupo hapa ili kuanza hatua za awali pia tumekuja kuona maeneo ya kufugia na kuweka kiwanda”, amefafanua Kawamala.

Amesema baada ya kuona maeneo wanataka kuwekeza katika ufugaji wa kisasa wa ng’ombe, ujenzi wa kiwanda cha kuchinja na kusindika nyama kwa viwango vya kimataifa.

“Kwa sasa baadhi ya Hoteli kubwa nchini Rwanda zimeanza kuagiza nyama kutoka nchi za Ulaya wakati tukifuga kisasa hapa Kagera tunaweza kuilisha Rwanda”, ameongeza Kawamala.

Mkuu wa Mkoa Gaguti amewakaribisha wawekezaji hao na kusema kuwa mkoa upo tayari kuwapa ushirikiano.

Amesema tayari amemwelekeza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NARCO Prof. Philemon Wambula pamoja na baadhi ya wataalam kutoka Sekretarieti ya mkoa kuwaonesha maeneo yaliyotengwa ili wakubaliane nayo na taratibu za kusajili kampuni na kuanza uwekezaji zianze mara moja.

“Baada ya Wiki ya Uwekezaji mwitikio umekuwa mkubwa sana wa wawekezaji kuja kwetu kuchangamkia fursa zilizopo Kagera na sisi tumejipanga tunawapokea na kuwaelekeza taratibu za uwekezaji, lakini jukumu letu ni kuhakikisha fursa zote ambazo wawekezaji wameziona wanazitumia katika uwekezaji ili kukuza uchumi wa mkoa wetu” ,amesema Gaguti.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni za Ranchi za Taifa (NARCO),Prof. Philemon Wambula amesema mkoa wa Kagera bado una fursa kubwa za uwekezaji katika sekta ya mifugo hasa katika viwanda vya kusindika nyama na maziwa pia uwekezaji katika malisho ya mifugo aidha, NARCO bado inayo maeneo makubwa ya kuwekeza. 
Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia jenerali Elisha Marco Gaguti akiwa na wafanya biashara kutoka Rwanda ofisini kwake leo.
Kiongozi wa wawekezaji kutoka nchini Rwanda William Kawamala akitoa zawadi kwa Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Elisha Marco Gaguti leo mkoani Kagera.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Elisha Marco Gaguti akiwa na wawekezaji kutoka Rwanda leo mkoani Kagera.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia jenerali Elisha Marco Gaguti akiwa katika picha ya pamoja na wafanya biashara kutoka Rwanda 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527