MRADI WA VECTORWORKS WAFIKIA TAMATI HUKU KIWANGO CHA MALARIA KIKIPUNGUA NCHINI


Mkurugenzi wa mradi wa VectorWorks Waziri Nyoni (kulia) akimkabidhi cheti maalum Msimamizi wa kitengo cha kudhibiti malaria nchini Winfred Mwafongo (kushoto) wakati wa halfa wa kumalizika mradi huo ambao umedumu kwa miaka mitano. VectorWorks imekuwa ikiendesha mradi wa kugawa vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu hapa nchini chini ya ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani – USAID kupitia Mfuko wa Raisi wa Marekani wa kudhibiti malaria.
**
MRATIBU wa Malaria kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,(TAMISEMI), Stella Kajange, amesema ugonjwa wa Malaria umepungua kwa asilimia 50 akimaanisha kuwa kiwango cha maambukizi ya vimelea vya ugonjwa huo vimepungua kutoka asilimia 15 kwa mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 7.3 kwa mwaka 2018.

Akizungumza na waandishi wa habari, wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani wakati wa mkutano wa wadau wa masuala ya malaria alisema kupungua kwa ugonjwa huo wa Malaria kumetokana na mafanikio waliyopata kati ya Serikali, wadau na wahisani wakiwemo. Alisema Tanzania inaendelea vizuri katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria ambao ugonjwa huo umekuwa ni tishio kwa jamii.

“Licha ya kupungua kwa ugonjwa huu nchini lakini ugonjwa huu bado ni tishio kwa jamii na hivyo serikali inaendelea na utekelezaji wa afua mbalimbali ili kuhakikisha tatizo hilo linapungua,”alisema Kajange.

Aidha aliongeza sera ya mwaka 2007 inaelezea muelekeo wa nchi katika kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa na afya njema ili waendelee na shughuli zao mbalimbali za uzalishaji na kujipatia kipato.

“Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo tunatekeleza sera mbalimbali kwa faida ya wananchi wetu kuhakikisha wanakuwa na afya njema,”alisema

“Serikali ya Tanzania inafanya kazi na wadau mbalimbali wa Maendeleo……tunawashukuru sana PMI kwa pamoja na USAID na wadau wengine kwa kutuunga mkono kwa miradi inayotekelezwa sehemu mbalimbali nchini,”alisema Kajange.

Naye Msimamizi wa Kitengo cha Kupambana na Malaria Mradi wa Taifa wa kudhibiti Malaria (NMCP),Winfred Mwafongo alisema ugonjwa wa Malaria unaathiri zaidi kundi la wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano.

Alisema katika mikakati yao waliyojiwekea ni kuhakikisha wanadhibiti Malaria nchini ambapo tayari wameweka utaratibu wa afua ambazo zinazohusika na udhibiti wa Malaria.

Alisema miongoni mwa afua hizo ni kuhakikisha kuna kuwepo na matumizi ya vyandarua vyenye dawa ,kuangamiza vijidudu na upuliziwaji wa viuadilifu kudhibiti mbu.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Mradi wa VectorWorks Waziri Nyoni alisema mradi huo umedumu nchini takribani miaka mitano ambao ulijikita katika usambazaji wa vyandarua vyenye dawa katika mikoa mbalimbali.

“Mradi umedumu nchini ndani ya miaka mitano na mwaka huu mwezi September ndio mwisho wa mradi huu,tunaamini kwa ushirikiano tulioupata umeweza kuleta tija kwa jamii katika kuhakikisha wananchi wanatumia vyandarua vilivyowekwa dawa,”alisema. 

Akizungumzia kuhusu uendelevu wa shughuli zilizokuwa zikitekelezwa na VectorWorks, Waziri Nyoni alisema kuwa “tumejenga mifumo thabiti ya kuhakikisha utaratibu wa ugawaji wa vyandarua kwa walengwa kupitia vituo vya kutolea huduma nchi nzima na kupitia shule za msingi katika mikoa 14, na uwajibikaji unaendelea bila changamoto yoyote, tumejenga uwezo wa bohari kuu ya dawa (MSD) kuendelea na utaratibu huu na pia watendaji ngazi za halmashauri wataendelea kusimamia utoaji wa huduma hizi hata bila uwepo wa VectorWorks ambayo ni mafanikio makubwa ya mradi” 

Aidha alisema nchini Tanzania mradi huo ulijikita katika maeneo matatu ikiwemo kushauri serikali juu ya sera zinazohusu masuala ya malaria, ,Utekelezaji wa afua ya ugawaji wa yyandarua vyenye dawa, kufanya tafiti juu ya ugonjwa wa malaria na upimaji wa matokeo ya program za malaria.

Mradi wa VectorWorks umekuwa ukifadhiliwa na USAID kupitia mfuko wa Rais wa Marekani wa kudhibiti Malaria (PMI).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527