SPIKA WA BUNGE AWASHAURI WABUNGE KUACHA KUFANYA 'NGONO KIHOLELA'.... WALE KWA NIDHAMU


Spika wa bunge la Uganda Rebecca Kadaga amewashauri wabunge wa Uganda na maafisa wa itifaki kulinda hadhi yao wakati wote wa Mkutano wa 64 wa Bunge la Jumuiya ya Madola.

Mkutano huo, uliopangwa kufanywa kati ya Septemba 22 na 29 mjini Kampala, unatarajiwa kuvutia wajumbe takribani 1,000 ambao unajumuisha maspika na wabunge kutoka mataifa yote 180 ya Jumuiya ya Madola.

Katika hotuba yake kwa wabunge na maafisa wa itifaki kabla ya mkutano huo, Kadaga alisisitiza kuwa nidhamu ni jambo la kwanza, kuheshimu kanuni kuhusu mavazi ya bunge na kuwatahadharisha kuhusu kujihusisha na ngono na wajumbe watakaofika, Gazeti la Observer la nchini humo limeripoti.

''Mnajua Watanzania walipokuja nchini humu (kupambana na Idi Amin,) kulipatikana watoto waliozaliwa hapa baba zao wakiwa raia wa Tanzania. Tunawajua mama zao lakini baba hatuwajui msijiingize matatani, Mwanaume kutoka Jamaica, utamuona lini tena? na kwa wanaume, mwanamke kutoka Pasifiki, Nauli lini utakwenda huko. Hivyo mnapaswa kuwa makini sana kwa kile mnachokifanya.'' alisema.



Kadaga ameona kuwa weledi unahitajika miongoni mwa maafisa wa itifaki katika kipindi hicho ili kuepuka mazingira yenye kukanganyana kati ya ujumbe na wenyeweji.

''Mtakapo wapeleka wageni kwenye vyumba vyao, simama mlangoni, unaweza kuingiza mizigo ukiwa sambamba na mhudumu wa hoteli. Fanyeni kazi yenu na muondoke,'' Kadaga alieleza.

Kadaga alisisitiza umuhimu wa kuwa na nidhamu ya kula (mezani) kwa wabunge na maafisa wa itifaki- akiwatahadharisha 'kutokujaza' sahani na kuchanganya kitindamlo (dessert) na chakula.

'Wakati wa kula, hata kama una njaa usiwe na pupa,'' alisema Kadaga, akieleza kisa cha mbunge mmoja ambaye aliambatana na raisi Yoweri Museveni alikabwa na kipande cha nyama.

Kwa mujibu wa Kadaga, Mbunge alipigwa mgongoni na kipande cha nyama kikaanguka mbele ya raisi wa Tanzania wakati huo Jakaya Kikwete, jambo ambalo liliaibisha ujumbe wa Uganda. Kadaga pia ameshauri kuepuka unywaji wa kupita kiasi wakati wa mkutano.

''Matumizi ya pombe yafanyike nyumbani na si kwa wingi, kuepuka harufu ya pombe asubuhi, kuna wakati tulikuwa na upungufu wa magari kisha tukaazima gari kutoka kwa mmoja wa wabunge, ilikuwa na chupa za bia na nyingine zikiwa zimemwagika na kumfikia spika wa Oman,'' alibainisha Kadaga.

Kadaga amesema mkutano huu ni mmoja kati ya matukio makubwa katika kuitangaza Uganda, na kile watakachokutana nacho wageni ndicho kitakachozungumzwa watakapotoka Uganda.

Ni miaka 52 tangu Uganda kwa mara ya kwanza ilipohodhi mkutano huu.

Afrika imehodhi mikutano 16, kenya mara tatu, Afrika Kusini mara mbili, Mauritius mara mbili, Uganda mara mbili, Nigeria mara mbili, Zambia, Namibia, Malawi,Cameroon na Tanzania mara moja.
CHANZO - BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527